Kwa ufupi
Kwa Watanzania wazalendo wanaolipenda taifa lao
hawakutakiwa kutumia Kiswahili kibovu. Hali hii ilileta aibu kwa taifa
letu kwani Redio One inasikilizwa na watu wengi hata nje ya mipaka yetu.
Lugha ya Kiswahili imekuwa ikiharibiwa siyo tu
na waandishi wa habari, bali pia na wazungumzaji, hasa watangazaji wa
redio na runinga.
Hivi karibuni nilikuwa na fursa ya kusikiliza
majadiliano katika vyombo vyetu vya habari kuhusu Ripoti ya Escrow
iliyotayarishwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC).
Ilitarajiwa kuwa majadiliano haya yangetoa picha kamili kuhusu
kilichojiri katika matumizi ya fedha zilizohifadhiwa katika Benki Kuu
kutokana na mzozo wa kifedha kati ya Shirika la Tanesco na IPTL.
Kwa kweli wananchi wengi hawajui kwa undani sakata
hili, hivyo kuwepo kwa kipindi katika redio zetu kunakuwa ni hatua
nzuri ya kuielimisha umma.
Suala la escrow liligusa hisia za watu wengi wa vijijini na mijini na walikuwa na hamasa kubwa kujua kilichoendelea bungeni.
Vikundi vya watu vilikusanyika kando ya redio na
runinga katika maeneo mengi nchini. Kwa hiyo kutoa ufafanuzi wa kina
kulisaidiia wananchi kupata ukweli ya mambo yaliyokuwa yakiendelea
bungeni.
Kinyume cha matarajio ya wengi, mjadala
uliofanyika tarehe 29/11/2014 kuanzia saa sita mchana hadi saa sita na
tano na dakika 49 usiku ulikuwa ni aibu tupu.
Ulikuwa ni wa aibu kwa sababu kilichojadiliwa hakikueleweka na kilikuwa ni upotoshaji uliokithiri.
Niseme tu kuwa Redio One ni redio inayoaminika
sana hapa nchini, pia nchi za nje kwa kutoa taarifa za matukio mengi
muhimu. Ilitarajiwa kuwa ingeweka heshima ya taifa letu kwa kuwa mfano
mzuri wa kutumia lugha sanifu na fasaha kwani Kiswahili ni lugha ya
taifa la Tanzania na lugha rasmi katika mawasiliano. Hata hivyo,
wazungumzaji walijieleza kwa kutumia Lugha ya Kiswahili iliyochanganyika
na Kiingereza.
Kwa Watanzania wazalendo wanaolipenda taifa lao
hawakutakiwa kutumia Kiswahili kibovu. Hali hii ilileta aibu kwa taifa
letu kwani Redio One inasikilizwa na watu wengi hata nje ya mipaka yetu.
Endapo watumiaji wa Kitanzania watatumia Kiswahili
kibovu itakuwa ni aibu kwa taifa. Nitatoa mifano michache ili
kuthibitisha malalamiko yangu.
Ningependa kuyahifadhi majina ya wahusika yaani mtangazaji na mzungumzaji na kijikita zaidi katika mazungunzo yao.
Mjadala uliokuwa ukiendelea, ulitumia Kiswahili
kilichochanganywa na Kiingereza, hali ambayo msikilizaji wa kawaida
hangeweza kuelewa kilichokuwa kikiendelea huko bungeni. Kwa maoni yangu
msikilizaji wa kawaida ambaye yuko kijijini, elimu iliyokusudiwa
kutolewa ingemsaidia kujifunza mambo mengi yanayoendelea nchini, lakini
waliambulia patupu. Majadiliano yaliyokuwa yakifanyika yalikuwa na
miundo ya sentensi kama ifuatavyo: Nafikiri this time masuala ya utaifa
yaliwekwa pembeni.
Yatupasa tukae sawa otherwise wengi watatulaumu. Let me tell you something.
Unajua sometimes tunatakiwa tujiweke sawa. Wako wasiosympathise na wewe.
Nafikiri this is best way kwa Watanzania kufikia
mafanikio. If they are trying to hide something they will see the
consequences. We can’t avoid this. Jana ilikuwa bombastic.
Kama inavyoonekana hapo juu, zipo sentensi ambazo
zina maneno ya Kiswahili na Kiingereza. Msamiati wa Kiingereza ni wa
kawaida na sikuona umuhimu wa kuacha maneno ya Kiswahili yanayoeleweka
na kutumbukiza maneno ya Kiingereza. Pia zilikuwapo sentensi ambazo
zilikuwa ni Kiingereza tu.
Kwa kweli taarifa walizokuwa wakijadiliana
zilikuwa ni muhimu. Naomba ifahamike kuwa ni lazima watangazaji wafahamu
kuwa wamefanya makosa makubwa.
Nafahamu wanao uwezo wa kuzungumza Kiswahili
fasaha kwani hakuna neno au msemo wa Kiingereza uliotumiwa ambao haukuwa
na tafsiri sahihi ya Kiswahili.
Jambo la msingi ni kuongeza juhudi ya kufikiri kwa
kina na kutafuta visawe vya maneno. Kwa mfano kusema ‘nafikiri this
time…’ ingeweza kusemwa, -‘Nafikiri wakati huu…’ Mifano mingine ni:
-‘ Yatupasa tukae sawa vinginevyo tutalaumiwa na
watu.” -‘Unajua wakati mwingine tujiweke sawa.’ -‘Nafikiri ni njia bora
kwa Watanzania kufikia mafanikio.’
-‘Kama unajaribu kuficha jambo utaona matokeo yake.’
- ‘ Hatuwezi kuepuka jambo hili.’
Ni matumaini yangu kuwa tutabadilika na kutumia Kiswahili fasaha katika vyombo vyote vya mawasiliano.
Wakereketwa na wapenzi wa Kiswahili wasisite
kuniletea mifano ya aina hii name nitakuwa tayari kuichapisha ili kwa
pamoja tuwakosoe wanaoidhalilisha lugha yetu.
0 Comments