“Bado kuna nafasi ya Bunge kufanya marekebisho. Hili linatakiwa kufanyika kama ambavyo tulikubaliana na Rais kupitia TCD”
James Mbatia
Kwa ufupi
MAMBO MANNE
- Ushindi wa urais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya 50
- Mgombea binafsi katika nafasi za udiwani, ubunge na urais
- Tume huru ya uchaguzi
- Urais kupingwa mahakamani
Dar es Salaam. Uamuzi wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa umewafungulia viongozi wa Ukawa kuishinikiza Serikali
kuiboresha Katiba ya sasa katika maeneo manne ili kuondoa mvutano katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mambo manne yanayodaiwa na Ukawa ambayo ni ushindi
wa urais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya 50, mgombea binafsi katika
nafasi za udiwani, ubunge na urais, tume huru ya uchaguzi na urais
kupingwa mahakamani ni yale yaliyoafikiwa baina ya Rais Jakaya Kikwete
na vyama vya siasa Septemba 8, mwaka jana.
Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia
amesema maboresho yaliyofanyika chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD) ni ya lazima ili kufanikisha uchaguzi huo kabla ya kupitishwa kwa
Katiba Mpya na kuondoa uwezekano wa vurugu.
Katika kikao hicho, Mbatia alisema walitiliana
saini kuwa iwapo uchaguzi wa mwaka huu utafanyika kwa kutumia Katiba ya
1977, Bunge lingekutana Novemba mwaka jana kufanya marekebisho hayo ya
15 ya Katiba na endapo hilo lingeshindikana, basi lingekutana Februari,
jambo ambalo pia halikufanyika.
Utekelezaji wa masuala hayo utawezekana iwapo
Serikali itawasilisha marekebisho hayo bungeni ili yajadiliwe kwa
dharura katika mkutano ujao wa Bajeti wa mwisho wa Bunge la Kumi, kwa
kuwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi ni kama haupo.
Alipoulizwa iwapo jambo hilo linawezekana katika
Mkutano wa Bajeti, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema:
“Ndiyo inawezekana. Serikali inaweza kuwasilisha jambo hili kwa dharura
na litajadiliwa na Kamati ya Uongozi, kama ikiona linafaa litapelekwa
bungeni kujadiliwa.”
Katika hilo Mbatia alisema: “Bado kuna nafasi ya
Bunge kufanya marekebisho. Hili linatakiwa kufanyika kama ambavyo
tulikubaliana na Rais kupitia TCD.”
Alisema ushauri wa TCD kwamba mchakato wa Kura ya
Maoni uahirishwe hadi mwakani umepuuzwa na matokeo yake yameonekana wazi
na kwa msingi huo, suala la kurekebisha maeneo hayo manne, si la
kupuuza hata kidogo.
“Hili lisipofanyika utaibuka mgogoro mkubwa.
Tatizo la Serikali yetu ni kutotaka kutekeleza mambo yanayoonekana wazi
kuwa na mkanganyiko, ndiyo sababu ya kukithiri kwa migogoro ya wakulima,
wafugaji, wafanyakazi na mingine mingi,” alisema Mbatia.
Dk Slaa akata tamaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema
endapo Serikali itashindwa kutekeleza makubaliano hayo, vyama vya
upinzani havina budi kuingia katika mapambano kwa katiba hiyohiyo.
“Kama hatumwelewi Rais Kikwete katika suala hili,
basi hatuwezi kumwelewa tena. Sioni juhudi zozote za Serikali kubadili
maeneo haya. Tulikubaliana naye mambo mengi lakini yote ameshindwa
kuyatekeleza, hata hili pia hawezi kulitekeleza,” alisema Dk Slaa.
Katibu mkuu huyo wa Chadema alisema umefika wakati wa vyama vya
upinzani kupambana hivyohivyo licha ya kuwapo tume ya uchaguzi isiyo
huru.
“Nimeshinda ubunge Karatu vipindi vitatu na tume
ikiwa ni hiihii. Wapinzani tuna wabunge zaidi ya 100, nadhani tupambane
tu,” alisema.
Alisema umefikia wakati wa kuing’oa CCM kwa
kutumia Katiba mbovu (iliyopo sasa) na kinachotakiwa kufanywa na vyama
vya upinzani ni kujipanga kuanzia vijijini hadi mijini ili kuzoa kura
zote.
“Tumeshinda Kawe, Ubungo, Mbeya Mjini na hata
Nyamagana. Tuache kulialia sasa, twende katika mapambano. Kwanza Bunge
lijalo ni la Bajeti na kwa vyovyote vile mabadiliko tunayoyataka
hayawezi kufanyika,” alisema.
Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Tanzania, Zitto
Kabwe alisema kinachotakiwa kufanywa sasa ni Baraza la Vyama vya Siasa
kuitisha mkutano wa vyama vyote ili kukubaliana mambo ya kuboresha
katika Katiba ya sasa.
“Jambo la pili ni Rais kuitisha Bunge kabla ya
kuanza kwa Bunge la Bajeti kujadili mabadiliko hayo na kuyapitisha ili
kuufanya uchaguzi mkuu uwe wa haki na huru,” alisema Zitto.
Juhudi za kumpata Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
George Masaju na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro
kuzungumzia hatua ambazo Serikali inachukua hazikuzaa matunda baada ya
simu zao kuita mara kadhaa bila kupokewa.
0 Comments