KICHEKO KWA WAFANYAKAZI


Kutokana na kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi kutopata fidia inayotokana na ajali mahala pa kazi, watumishi kutoka sekta zote wataanza kunufaika na mfuko wa fidia nchini

Arusha. Kutokana na kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi kutopata fidia inayotokana na ajali mahala pa kazi, watumishi kutoka sekta zote wataanza kunufaika na mfuko wa fidia nchini

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Anthony Mavunde alisema jana kuwa fidia kwa wafanyakazi zitaanza kulipwa kuanzia Julai mosi.

Mavunde alisema hayo wakati wa akifungua semina kuhusu mfuko huo ambao umetokana na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ya mwaka 2008.

Alisema kwa sasa mfuko umeboreshwa badala ya kutoa fidia elekezi ya Sh10,800, lakini mfanyakazi atalipwa zaidi ya fedha hizo.

“Mfuko huu hautachangiwa na wafanyakazi, bali waajiri ndiyo watachangia asilimia ambayo itamwezesha mfanyakazi kulipwa fidia atakapokutwa na majanga,” alisema Mavunde.

Pia, alisema licha ya mfuko huo kuanzishwa unakabiliwa na upungufu wa madaktari waliobobea juu ya masuala ya ajali na ugonjwa kazini na kuwataka madaktari kuzingatia weledi wa kazi kutoa taarifa sahihi kwenye mfuko huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Masha Mshomba alisema tangu mfuko huo uanzishwe mwaka 2015 walipanga kutoa mafunzo kwa zaidi ya madaktari 300 mpaka ifikapo Julai, mwaka huu.

Alisema lengo ni kuhakikisha mafunzo juu ya mfanyakazi yupi alipwe fidia yanatolewa ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria hiyo unafanikiwa.

“Lengo la semina hii ni kubaini magonjwa yatokanayo na kazi, ajali na vifo vitokanavyo na kazi. Hatuwezi kujua bila kuwapo na taarifa ya daktari, tunaamini madaktari ni wadau na watakwenda kutusaidia katika utendaji wa mfuko huu ili uwe na manufaa kwa wahusika,” alisema Mshomba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa mfuko huo, Emmanuel Humba alisema utajumuisha mifuko yote ambayo ilitangulia kuanzishwa kama mfuko wa pensheni, bima ya afya na mingine na lengo ni kufanya mafao yawe yanatolewa sehemu moja.

Baadhi ya wafanyakazi wamesema wana imani mfuko huo utasaidia kuondoa ukiritimba uliopo.

“Tofauti na zamani, mtu alikuwa analazimika kwenda huku, mara kule mara apigwe kalenda, lakini nadhani hawa watakuwa tofauti. tunawaomba wawe wanafanyia kazi haraka madai,” alisema Lucas Ntumba wa Kampuni ya Tanzania Spread Sheet Ltd.

0 Comments