MAUAJI HAYA YANATUTISHA



Kuanzia Januari hadi Mei, zaidi ya watu 18 wameuawa mkoani Mwanza katika matukio ya kiuhalifu, ikiwamo kuvamiwa na kupigwa risasi au kucharangwa mapanga.

Kwa lugha nyepesi mtu unaweza kusema Mwanza siyo eneo salama kuishi kwa watu wa kada zote, kuanzia wafanyabiashara na wananchi wa kawaida kutokana na matukio ya kihalifu yakiwamo mauaji.

Kuanzia Januari hadi Mei, zaidi ya watu 18 wameuawa mkoani Mwanza katika matukio ya kiuhalifu, ikiwamo kuvamiwa na kupigwa risasi au kucharangwa mapanga.

Matukio hayo ni pamoja na yale ya wafanyabiashara wa maduka ya fedha kwa njia ya mtandao kuvamiwa, kuporwa, kujeruhiwa na baadhi kuuawa kwa kupigwa risasi.

Zaidi ya watu 10, wamepoteza maisha katika matukio ya uvamizi kwenye maduka hayo.

Wimbi hilo la mauaji limeingia hadi katika maeneo ya ibada, baada ya watu wasiofahamika kuingia katika Msikiti wa Rahman kata ya Mkolani na kuwaua kwa kuwacharanga mapanga watu watatu, akiwamo imam wa msikiti huo, Sheikh Feruz Ismail na waumini wengine wawili.

Kama hiyo haitoshi, siku nne tu baada ya tukio la waumini kuuliwa, Mei 22, watu wasiojulikana walimuua kwa kumpiga risasi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bulale kata ya Mhuongwa, Alphonce Nyinzi na kumjeruhi Neema Marangula katika kiganja cha mkono wa kulia.

Awali, Mei 11, katika Kijiji ch Sima Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, watu saba wa familia ya Zakaria Mbata, waliuawa na watu wasiojulikana kwa kukatwa mapanga akiwamo mama wa familia hiyo, Eugenia Philipo na watoto wake watatu. Wauaji hao pia, waliwaua wageni watatu wa familia hiyo.

Nimelazimika kuorodhesha matukio haya kuonyesha uzito wa mauaji ya kinyama yalitokea mkoani Mwanza, ndani ya miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella katika kikao chake cha kwanza na watendaji wa Serikali na vyombo vya dola, aliagiza kila mmoja kutimiza wajibu wake kulinda usalama wa raia na mali zao.

Alisema haiwezekani jiji kama Mwanza wafanyabishara wafunge biashara zao saa 12:00 jioni na wananchi kulazimika kujifungia ndani kwa hofu ya kuvamiwa na majambazi

Sifa ya jiji ni kuuwapo kwa huduma kama ya maduka ya biashara yakiwamo ya fedha kwa saa 24.

Mongella aliagiza halmashauri zote za wilaya mkoani Mwanza kuajiri askari mgambo kati ya 200 hadi 300, watakaoshirikiana na askari polisi pamoja na kamati za ulinzi za mitaa na vijiji kudumisha amani na usalama.

Kauli ya Mongella ilipigiwa chapuo na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga aliyebainisha kuwa Serikali tayari imegundua kuwapo mitandao saba ya uhalifu mkoani Mwanza na kwamba miwili imesambaratishwa, huku juhudi zikiendelea kukabili iliyosalia.

Kama alivyosema Mongella, vyombo vya dola vinapaswa kutimiza wajibu kwa kukabiliana na wahalifu.

Polisi hawana sababu wala udhuru, kwa nini wawache majambazi watambe kwa kupora na kuua wananchi kila kukicha?

Ni majuzi tu, Jeshi la Polisi limepewa vifaa na zana za kazi yakiwamo magari ya kisasa, ambayo yote yamegharamiwa kwa kodi za wananchi ambao sasa wanaogopa kushiriki shughuli za uzalishaji kwa kuhofia majambazi.

Hii haikubaliki hata kidogo, askari sharti watimize wajibu wa kulinda raia na mali zao siyo kwa kudhibiti ujambazi pekee, bali hata mauaji ya vikongwe yaliyoshtadi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Hata ukataji wa viungo na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ulianzia katika mikoa hii.

Ngollo John ni mwandishi wa gazeti hili mkoani Mwanza, anapatikana kwa baruapepe: maoni@mwananchi.co.tz

0 Comments