WATU 11 wamekufa papo hapo na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizotokea sehemu moja, zikihusisha basi la abiria, lililopamia malori mawili ya mizigo yaliyogongana uso kwa uso na kuungua moto eneo la Dakawa – Veta, wilayani Kilosa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema mjini hapa jana kuwa ajali ya kwanza, malori mawili ya mizigo yaligongana uso kwa uso juzi saa 12 jioni na kuwaka moto.
Katika ajali hiyo ya juzi jioni, lori la mizigo aina ya Scania ambalo namba za mbele hazikutambuliwa, lakini tela lake ni namba T 704 CEC, likitoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa, liligongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso yenye namba za usajili T 963 BLW, lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Kamanda Matei alisema katika ajali hiyo, watu watano walipoteza maisha papo hapo kwa kuungua moto mpaka ikashindikana kuwatambua, akiwemo dereva wa bodaboda aliyekuwa pembeni mwa barabara na pikipiki yake katika eneo la tukio.
Wengine waliokufa papo hapo na kushindwa kutambulika kwa mujibu wa Kamanda Matei, ni madereva wa malari hayo na wasaidizi wao wawili; mmoja kwa kila lori.
Alisema chanzo cha ajali hiyo, ni kutokana na gari ndogo iliyokuwa mbele ya Fuso hilo kusimama ghafla na kusababisha dereva wa Fuso kupita pembeni bila kuangalia mbele na kugongana uso kwa uso na Scania yenye shehena ya mafuta na kusababisha malori hayo kuwaka moto.
Wakati malori hayo yakiwa eneo la tukio, jana alfajiri kulitokea ajali nyingine ambapo basi la abiria mali ya Kampuni ya Otta Classic yenye namba za usajili T 201 DGK aina ya Higer, liliparamia moja ya malori yaliyokuwa yamepata ajali katika eneo hilo na kuua watu sita papo hapo na kujeruhi wengine 44.
Kamanda Matei alisema kati ya majeruhi hao, sita hali zao ni mbaya na walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro kupatiwa matibabu zaidi. Alisema ajali hiyo ilitokea saa 10 alfajiri ya Julai Mosi mwaka huu, wakati basi hilo likitokea Bukoba mkoani Kagera kwenda Dar es Salaam.
Waliokufa katika ajali hiyo kwa mujibu wa Kamanda Matei ni dereva wa basi hilo, msaidizi wake, kondakta na abiria wengine watatu.
Alitaja majina ya waliokufa kuwa ni Yassin Mgongolwa (41) dereva wa basi hilo, Veronica Jeremia ambaye ni kondakta, Said Shomari Simba (30) dereva msaidizi na abiria Lilian Paul (34), Jonia Kokumbuga na mwamamke mwingine mwenye umri kati ya miaka 30 -35, ambaye hajatambulika.
Miili ya marehemu hao na maiti zilizoungua na kushindwa kutambuliwa, imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.
Kamanda Matei alisema kabla ya basi hilo kupata ajali, lilisimamishwa na askari wa usalama barabarani, lakini dereva alikaidi na kupitiliza na baada ya muda likapata ajali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, ambaye pia alifika eneo la tukio hilo jana, alisema miili iliyoungua, itatambuliwa kwa kutumia vinasaba (DNA) na kuwataka ndugu na jamaa zao kuwa na subira wakati utambuzi huo utakapofanyika.
Alilipongeza Jeshi la Polisi mkoa na vikosi vya Zimamoto na wananchi wa vijiji vya karibu na eneo la ajali kwa kusaidia kuzima moto na kuokoa majeruhi wa ajali hiyo.
0 Comments