MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), imebuni kifaa cha kudhibiti wizi wa magari na pikipiki za abiria maarufu bodaboda, kwa kutumia simu.
Kwa kutumia kifaa hicho, dereva atakuwa na uwezo wa kuzima pikipiki au gari kwa kutumia simu ya mkononi, ambayo namba yake itakuwa imefungwa katika chombo hicho cha usafiri.
Akizungumzia kifaa hicho, Mwalimu wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Veta, Valerian Sanga alisema alishirikiana na mwalimu mwenzake wa chuo hicho anayefundisha masuala ya umeme, Christian Brighton kubuni kifaa hicho kilichowachukua miaka miwili kukamilika.
“Wiki tatu zilizopita ndio tumekamilisha kifaa hiki na kuanza kufanya kazi, tukafunga kwenye pikipiki hii (akionesha) kupima na kuonesha watu namna ya kuweka ulinzi kwenye vifaa vyao kwa kuwa mifumo kama hii, inauzwa katika kampuni za nje lakini ni gharama sana,”alisema.
Mwalimu huyo anatoka Kituo cha Veta Kipawa jijini Dar es Salaam, ambacho kilibuni mfumo huo ili kudhibiti wizi wa pikipiki.
Ubunifu huo ulichangia mamlaka hiyo, kupata tuzo ya mshindi wa jumla wa Maonesho ya Kimataifa ya 40 Dar es Salaam, yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Sanga alisema kifaa hicho kina GPS na kinatumia mawasiliano ya simu kwa kutumia GSM, itakayo saidia kujua sehemu pikipiki au gari lilipo, lakini pia kikimwezesha mmiliki kuzima nakuwasha usafiri wake popote ulipo.
“Unatumia simu ya mkononi ambayo namba zako zinakuwa zimefungwa katika chombo cha usafiri, ili zikuwezeshe kuzima kama kimeibiwa ambapo baada ya dakika tano kitazima na hakitawaka mpaka utume tena ujumbe wa kutaka iwake,” alisema.
Sanga alisema kwa sasa wanafunga kifaa hicho kwa gharama ya Sh 400,000, lakini anatarajia baadaye watakapopata oda nyingi, watapunguza bei kwani kwa siku nne tangu kuanza maonesho hayo wameshapata watu wengi wanaohitaji.
“Tunategemea kupata watu wengi wanohitaji na tayari watu wawili; mmoja ana pikipiki ishirini na mwingine kumi, wametaka tuwafungie huku tukiamini mpaka maonesho yaishe tutapata wengi zaidi,”alisema.
Alisema ili kukidhi mahitaji hayo, wamekuwa wakifundisha wanafunzi wa chuo hicho ili washirikiane katika kutengeneza vifaa hivyo kwa wingi ikiwa watajitokeza wengi wanaozihitaji.
Baadhi ya watu waliotembelea kuona pikipiki hiyo, walishangazwa na utaalamu huo kufanyika nchini na kutaka serikali kusaidia, hususani wakati huu wa taifa linapojiandaa kwa uchumi wa viwanda.
Mmoja wa wananchi hao, Godwin Mlulu alisema kifaa hicho kimekuja wakati muafaka kutokana na kukithiri kwa wizi wa pikipiki. Lakini alipendekeza bei ipunguzwe, kwa kuwa wamiliki wengi wa pikipiki za biashara, ni wenye kipato cha chini.
0 Comments