WIZARA ya Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu imetaka wananchi kuepuka kampuni za uwakala wa ajira nchini ambazo hutangaza nafasi za ajira huku zikiwataka waombaji kulipia ili kusailiwa.
Msemaji wa Wizara hiyo, Ridhiwan Wema jana alisema kampuni za namna hiyo hawazitambui na hivyo hazina usajili wa kufanya shughuli hiyo nchini.
“Hizi kampuni sisi hatuzitambui, mtafuta kazi hatakiwi kutozwa fedha isipokuwa kampuni inaingia makubaliano na mwajiri ambaye amempa kazi ya kumtafutia wafanyakazi,” alisema Wema.
Alitaka wananchi wawe makini na wasikurupuke kutuma maombi kabla ya kujiridhisha kama kampuni zimesajiliwa na ili kupata taarifa sahihi, mwombaji anaweza kufika Wizara ya Kazi na kuuliza, kwa kuwa wao ndio wasajili pia wakibaini uwepo wa kampuni hizo watoe taarifa wizarani na Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Aidha, aliwasihi wananchi hususan vijana, wasiwe wepesi kulipia gharama, kwa sababu huduma ya ajira haipaswi kutozwa fedha kwa kuwa si haki kutoa kazi kwa masharti ya kulipwa, hali ambayo inaashiria vitendo vya rushwa.
Wema alibainisha kuwa kampuni zinazofanya shughuli za uwakala wa ajira nchini zimesajiliwa na Wizara ambapo moja ya masharti yanayotakiwa kuzingatiwa ni pamoja na kutowatoza waombaji wa nafasi za ajira zinazotangazwa.
Alisema kuna vigezo vingine pia vinavyozingatiwa, ili kukidhi usajili ambapo huainishwa kwa majina na taarifa za mahali pa kudumu zilipo ofisi za kampuni na kufahamu kama zimesajiliwa kwenye mamlaka husika, mfano Brela, hayo yote ni kwa ajili ya kufanya urahisi wa kizifuatilia pindi kunapozuka utata.
Aliongeza kwamba vigezo vingine ni kujiridhisha kama ina wataalamu wa kutosha kwenye masuala ya ajira, ambapo baada ya kujiridhisha husajiliwa na kuzitangaza kwenye vyombo vya habari.
Wema alitaka wananchi watambue kuwa kampuni zinazotangaza nafasi za ajira huku zikitaka waombaji walipie fedha kwa ajili ya usaili si salama kwao, hivyo wanatakiwa kuepukana nazo na kutoa taarifa.
Nuh Yusuf ambaye ni Ofisa wa kampuni ya Zoom ambayo ni wakala wa ajira nchini, alisema sababu kubwa ya kuendelea kwa utapeli wa mtandao ni kukosekana kwa ushikiano wa karibu na vyombo vya sheria hususan Jeshi la Polisi katika kudhibiti suala hilo.
“Tumejaribu kufuatilia suala hilo TCRA kitengo cha TZ-CERT, tukashauriwa twende Polisi na mmoja ambaye alipatwa na hilo tatizo, tulipofika kituo cha Polisi cha Oysterbay hawakuonesha ushirikiano wowote,” alisema Yusuf.
0 Comments