HONGERA KILIMANJARO QUEENS


Kwa ufupi

Shujaa wao alikuwa Mwanahamisi Omari aliyefunga mabao mawili na kuipeleka timu hiyo mapumziko ikiongoza 2-0 dhidi ya Harambee Starlets iliyopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa mashindano yaliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Dar es Salaam. Kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu imewabeba kinadada wa Tanzania, Kilimanjaro Queens kwenye dhihaka ya kuwa kichwa cha mwendawazimu kimataifa baada ya kuibwaga Harambee Starlets ya Kenya kwa mabao 2-1 na kutwaa ubingwa wa kwanza Kombe la Chalenji kwa Wanawake kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Shujaa wao alikuwa Mwanahamisi Omari aliyefunga mabao mawili na kuipeleka timu hiyo mapumziko ikiongoza 2-0 dhidi ya Harambee Starlets iliyopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa mashindano yaliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Mabingwa hao wapya waliifutia machozi Tanzania ya aibu baada ya mwakilishi wake mwingine, timu ya soka ya wanawake ya Zanzibar kugeuzwa kapu la mabao kwa kutunguliwa 30 katika mechi tatu ilizocheza kwenye mashindano hayo yakiwamo 11-0 dhidi ya Kenya.

Katika mchezo huo wa fainali uliofanyika kwenye Uwanja wa kituo cha Ufundi cha Njeru, Jinja, Kili Queens imeutwaa ubingwa ikionyesha kiwango kikubwa katika mchezo huo na kuidhibiti vilivyo Kenya.

Mwanahamisi Omari, aliwapa furaha Watanzania akifunga mabao dakika ya 28 na 43, huku lile la kufutia machozi la Kenya likifungwa dakika ya 48 na Christine Nafula.

Kili Queens ilipata bao la kwanza baada ya kugongeana vizuri na Mwanahamisi kuunasa mpira na kumalizia wavuni kwa shuti la kawaida, huku la pili likifungwa kwa shuti kali kutokana na juhudi za mchezaji huyo aliyepachikwa jina la Gaucho kutokana na soka lake wakimfananisha na mshambuliaji wa zamani wa Brazil, Ronaldinho Gaucho.

Kipindi cha pili, Kenya walirejea kwa nguvu na kupata bao la kufutia machozi lililofungwa dakika ya 48 na Christine Nafula.

Kuingia kwa bao hilo kuliwazindua Kili Queens ambao walilishambulia lango la Kenya, lakini uimara wa kipa Vivian Akinyi uliwaokoa Kenya kwani safu ya ushambuliaji iliyoongozwa na Gaucho, Asha Rashid ‘Mwalala’ ilikosa mabao dakika ya 41, 53 na 75. Katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, Ethiopia iliichapa Uganda Crested mabao 4-1.

Kikosi :

Kili Queens: Fatuma Omari, Asha Rashid, Anastazia Anthony, Fatuma Issa, Mwanahamisi Omari, Donisia Daniel, Fatuma Bushiri, Amina Ally, Stumai Abdallah, Wema Richard na Maimuna Khamis.

0 Comments