PASIPOTI ZA TANZANIA ZAADIMIKA

Uhamiaji haiwezi kukwepa lawama kuadimika kwa pasipoti

Kwa ufupi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alinukuliwa kwenye habari hiyo akisema Serikali ilikuwa imelipia vitabu hivyo na juzi Idara ya Uhamiaji ilikuwa imevipokea na kwamba mpango wao wanataka hadi kufika Desemba, wawe wametengeneza vitabu 79,000.

Gazeti hili toleo la jana kwenye ukurasa wake wa pili kulikuwa na habari iliyohusu Idara ya Uhamiaji kupokea vitabu 10,000 vya hati za kusafiria au pasipoti, vilivyoadimika kwa kipindi cha miezi mitatu.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alinukuliwa kwenye habari hiyo akisema Serikali ilikuwa imelipia vitabu hivyo na juzi Idara ya Uhamiaji ilikuwa imevipokea na kwamba mpango wao wanataka hadi kufika Desemba, wawe wametengeneza vitabu 79,000.

Kauli ya Mwigulu inagongana na aliyoitoa Katibu Mkuu wake, Meja Jenerali Projest Rwegasira ambaye alisema matatizo hayakuwa upande wa Serikali, bali kwa kampuni iliyopewa zabuni hiyo.

Hati za kusafiria ni utambulisho wa lazima kwa raia wa nchi yeyote anaposafiri kwenda nchi nyingine. Kwa maana hiyo, ni haki ya kila Mtanzania kuwa nayo pale anapohitaji kusafiri.

Lakini pamoja na maelezo hayo inashangaza kuona kwamba waziri, naibu wake, katibu mkuu na kaimu kamishna wa Uhamiaji wamekaa kimya kwa miezi yote mitatu na hakuna aliyejitokeza kutoa maelezo yeyote.

Kwa muda wote huo, wananchi waliokuwa na safari mbalimbali za kwenda nje ya nchi walipata usumbufu mkubwa ambao ama usingekuwapo au usingekuwa mkubwa kama kungekuwa na taarifa za kina na za wazi kuhusu suala hilo.

Viongozi hao wameibuka baada ya kufuatwa na vyombo vya habari na pengine ndiyo maana maelezo yanakinzana; waziri anazungumzia malipo lakini katibu mkuu anazungumzia tatizo la mzabuni.

Waandishi wetu walianza kufuatilia habari hiyo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi waliokuwa wakihitaji hati hizo kwa ajili ya safari mbalimbali na kukabiliwa na usumbufu mkubwa.

Kama ilivyothibitishwa baadaye na Serikali, hati ya za kusafiria zilikuwa zikitolewa kwa waombaji waliokuwa na safari za dharura tu na ambao walitakiwa kuwasilisha hoja zao kwa kamishna wa Uhamiaji.

Kutokana na kutokueleweka vyema kwa tatizo hilo na hatua zilizokuwa zimechukuliwa, utaratibu huo uliibua manung’uniko kutoka kwa baadhi ya waombaji kila mmoja akisema lake kuhusu kuandimika kwa hati hizo.

Kuna Watanzania walitakiwa kusafiri nje katika kipindi hicho kwa sababu tofauti, ikiwamo matibabu, biashara, masomo na kushiriki mikutano ya kimataifa na kwa kila mmoja, safari hizo zilikuwa na umuhimu mkubwa.

Kwa kusimamisha safari kwa miezi mitatu bila ya kujali kama zilikuwa za dhadhura au la, huenda athari mbalimbali zilijitokeza kwa mtu mmoja mmoja au hatua taasisi hivyo ilitarajiwa kwamba idara hiyo ingetoa kwa wakati, taarifa ili wahusika wajipange na pia kuondoa malalamiko.

Kuadimika kwa vitabu vya hati za kusafiria siyo dhambi hasa ikiwa kuna sababu za msingi zilizochangia uhaba huo.

‘Hapa Kazi Tu’ ndiyo kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano. Kama ambavyo Rais John Magufuli anavyoitekeleza kwa vitendo na hata mawaziri na viongozi wengine, tunatarajia pia hata taasisi na idara za Serikali kama hii ya Uhamiaji inapaswa kuitekeleza siyo kimyakimya tu, bali kwa uwazi.

Hii ni changamoto ambayo tunadhani kwamba vitengo vya mawasiliano vinapaswa kuichukua kwa uzito mkubwa na kuifanyia kazi ili isitie doa kazi nzuri inayofanywa. Maoni ya mhariri Mwananchi

0 Comments