Walimu wa Shule ya Sekondari Hasanga, iliyopo wilayani Mbozi mkoani Songwe na wafanyabiashara wawili, wanahojiwa na vyombo vya usalama mkoani Mbeya kwa tuhuma za kuhusika na utengenezaji wa mitihani feki ya kidato cha nne.
Watuhumiwa hao, James Kapinga (36) ambaye anadaiwa kufanya kazi Shule ya Sekondari ya Hasanga pia anajitolea kufundisha Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Sangu, Baraka Mwazambe (28), mfanyabiashara na mkazi wa Tunduma na mtaalamu wa masuala ya Tehama (IT), Alex Mochi.
Watu hao kwa pamoja inadaiwa walikamatwa juzi usiku baada ya mwanafunzi mmoja ambaye jina lake na la shule vimehifadhiwa kukutwa na mtihani wa somo la Kiingereza na alipobanwa, inadaiwa aliwataja wahusika hao.
“Mwanafunzi huyu ni wa shule nyingine tena si ya Mbeya, alikutwa na mtihani feki wa somo la Kiingereza, alipohojiwa alieleza mtihani huo ulitoka Mbeya na Serikali ilipofuatilia iliwabaini wahusika ambao walikuwa wanasambaza mitihani feki,” kilisema chanzo kimoja cha habari hii.
Akizungumzia sakata hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja, alikiri ofisi yake kupokea taarifa juu ya uvujaji wa mitihani na walipofuatilia walibaini mitihani hiyo ni feki.
“Mbeya hakuna mitihani iliyovuja kama inavyoelezwa katika mitandao, ukweli ni kwamba suala hilo lilifuatiliwa ilibainika mitihani inayosambazwa si ile iliyochapishwa na Baraza la Mitihani la Taifa, ni feki na baadhi ya wahusika wanahojiwa na vyombo vya dola,”alisema.
Naye Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Benedict Sandy, alisema hakuna mitihani iliyovuja.
“Mitandao imekuwa ikitoa taarifa za upotoshaji eti mitihani imevuja, mitihani iliyosambaa na kukutwa na baadhi ya wanafunzi tena si wa Mkoa wa Mbeya ni feki na wahusika wanaodaiwa kuisambaza wamekamatwa.
“Nawaomba wanafunzi wazingatie yale waliyofundishwa, mitihani hiyo inakuja kwa lengo baya la kuwapotezea muda wao na mwisho wa siku kuishia kufeli, watu wanaofanya kazi hiyo wapo kimasilahi,”alisema.
0 Comments