Mwalimu akithaminiwa elimu yetu itapanda chati
Kwa ufupi
Ukisoma hotuba zake nyingi, zimezungumzia kwa kina masuala ya elimu kama mkombozi. Mwalimu alieleza wazi kuwa, lengo la kwanza la elimu ni kumkomboa mtu binafsi na taifa kutoka kwenye kutegemea mataifa yaliyoendelea kiuchumi na kiutamaduni.
Mwaka 1966, Mwalimu Julius Nyerere alisema, nanukuu.
“Wale wenye wajibu wa kufanya kazi na vijana wa umri mdogo wana nguvu kubwa zisizozidiwa na nguvu za yeyote yule kwa kutilia maanani hali ya baadaye ya jamii yetu. Nguvu hizi zipo katika makundi mawili, wazazi na walimu.”
Ukisoma hotuba zake nyingi, zimezungumzia kwa kina masuala ya elimu kama mkombozi. Mwalimu alieleza wazi kuwa, lengo la kwanza la elimu ni kumkomboa mtu binafsi na taifa kutoka kwenye kutegemea mataifa yaliyoendelea kiuchumi na kiutamaduni.
Aidha, elimu inapaswa kumjengea mhitimu maarifa, stadi na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha halisi anayoishi.
Katika kufanikisha lengo hili la elimu, mwalimu alitaja katika nukuu hapo juu kuwa kuna makundi mawili ambayo yana nguvu kubwa ya kuwafanya wanafunzi kufikia malengo ya kuwapo shuleni. Makundi haya ni wazazi na walimu.
Tafiti nyingi zilizofanyika katika kubaini sababu za kushuka kwa ubora wa elimu zimekuwa zikijikita katika kuangalia masuala kama miundombinu isiyofaa ya kufundishia na kujifunzia. Ni tafiti chache zilizolenga kuangalia ubora wa walimu na mazingira yanayomzunguka.
Pia, tafiti hizo zinaonyesha wazi kuwa watoto wetu hawajifunzi licha ya kuwa wanakwenda shuleni. Kwa mfano, siyo jambo la kushanganza kuona watoto wakimaliza darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika.
Jitihada zilizofanyika kujaribu kuinua kiwango cha ubora wa elimu haziwezi kupuuzwa hata kidogo. Serikali na wadau mbalimbali wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kuinua kiwango cha ubora wa elimu yetu, lakini bado hatujaweza kupata matokeo yanayotakiwa kama ambavyo wadau wengi walitarajia.
Lazima tukubali kutafuta mzizi halisi wa tatizo la kushuka kwa elimu yetu. Pengine tatizo linafahamika lakini nia ya kushughulikia tatizo siyo makini.
Kimsingi, tumechelewa kushugulikia kiini cha tatizo kiasi kwamba Tanzania ya viwanda na ya uchumi wa kati tunayoitaka kufikia mwaka 2025, inaweza kuishia midomoni kama hatutaamua kuchukua hatua mapema.
Wadau wengi wa elimu wameshasema kuwa kuwathamini walimu ni moja ya hatua ya kurejesha ari ya ufundishaji kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, yaani enzi za Mwalimu Nyerere.
Kuanzia ngazi ya taifa mpaka familia, walimu hawaonekani tena kama watu muhimu; wanachukuliwa kama watu maskini waliokosa cha kufanya na ndiyo maana wapo huko.
Mwalimu mmoja aliwahi kusema: “Kuna wakati wanafunzi wananiuliza, “Mwalimu, una akili, lakini sasa kwa nini uliamua kuwa mwalimu?” Maswali ya aina hii yanakera. Ina maana wanaamini mwalimu ni mtu aliyefeli, asiye na akili.
‘’Ninapowaambia, nilipenda tu kuwa mwalimu”, wananiambia huoni kwamba unachelewa katika maisha? Haya ndiyo maisha tunayoishi katika shule hii.’’
Ni dhahiri kuwa huu ndiyo mzizi wa tatizo la kushuka kwa ubora elimu yetu. Miundombinu ni muhimu katika kujifunza na kufundisha, lakini pasipo walimu bora wenye moyo na hamasa ya kufundisha kamwe hatutofikia elimu bora tunayoitaka.
Utafiti uliofanywa na shirika la HakiElimu mwaka 2011 usemao: Je? Walimu wana sifa za ualimu na hamasa ya kufundisha?, pamoja na mambo mengine ulibianisha kuwa mwalimu kuwa na sifa nzuri za kitaaluma pekee bila kuwa na hamasa na moyo wa kujitolea hakusababishi kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi kitaaluma kuimarika’
Benedicta Mrema ni ofisa programu Idara ya Habari na Utetezi, HakiElimu media@hakielimu.org
0 Comments