WANAOSOMA NJE YA NCHI WAJITEGEMEE- HESLB


Watanzania waliopata ufadhili wa kusoma nchini China, hawatapata mikopo baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwaondoa kwenye orodha ya wanufaika. 

Taarifa iliyotolewa na HESLB, ikijibu Ubalozi wa Tanzania nchini China, kuhusu madai ya kuchelewa kwa fedha za mikopo kwa wanafunzi wanaosoma nchini humo imeeleza kuwa hatua hiyo inatokana na maelekezo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwamba wanafunzi wote wanaopata ufadhili kutoka nchi rafiki watajitegemea ikiwamo gharama za tiketi za ndege.

Barua hiyo ya Desemba 20, 2016 iliyomnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul Razaq Badru inaeleza kuwa mwaka huu wanafunzi hao hawatanufaika na mikopo kama ilivyokuwa ikitolewa miaka ya nyuma.

Jana, akizungumza na waandishi wa habari, Badru aliitambua barua hiyo huku akisita kutolea ufafanuzi wake kwa madai ilikuwa ni majibu kwa wanafunzi hao wa China.

Hata hivyo, alisema endapo kutakuwa na madai kutoka kwa wanafunzi hao watalazimika kutolea ufafanuzi.

Akizungumzia suala hilo Naibu Waziri Elimu, Stella Manyanya alisema ni hekima zaidi kuangalia au kusaidia wanafunzi wa ndani wasiokuwa nacho kuliko wanaopata ufadhili wa nje ya nchi.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul Razaq Badru ameunda kikosi maalumu (Task force) kwa ajili ya msako wa kuwanasa waajiri sugu wote nchini wasiowasilisha makato na majina ya wanufaikaji wa mikopo ya bodi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Badru amesema kikosi kazi hicho kitaanza kazi Januari 2, mwaka 2017 na kitafanya kazi hiyo kwa siku 14 mfululizo wakipita ofisi moja baada ya nyingine.

Amesema wadaiwa sugu ni wale walioshindwa kurejesha kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10. Kiasi kilichokusanywa na Bodi hiyo hadi sasa ni Sh 140bilioni kati ya Sh300bilioni na deni linalodaiwa ni Sh160bilioni.

0 Comments