SIMULIZI

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Kwa ufupi

Nimeambiwa kuwa moja ya sababu kubwa ya usultani ule kuwa maarufu na nguvu zaidi ni kafara za kuchinja watu zilizofanywa waanzilishi wake.

Kule kwetu Tunduru mkoani Ruvuma kuna viongozi wa jadi wanaitwa Masultani. Sitotaja majina ya sultani hizo nisije nikatengwa, lakini moja ya himaya kuu za usultani, kubwa na maarufu, ina makao yake makuu kijijini kwetu.

Nimeambiwa kuwa moja ya sababu kubwa ya usultani ule kuwa maarufu na nguvu zaidi ni kafara za kuchinja watu zilizofanywa waanzilishi wake.

Nimewahi kuhadithiwa kuwa kila sultani mpya anayekuja katika mnyororo huo anarithi vitu kadhaa ambavyo ndiyo alama ya usultani ule na kwamba baadhi ya vitu hivyo ni mabaki ya watu waliotolewa kafara. Pamoja na urithi huo wa siri, pia sultani mpya hupewa miiko kadhaa.

Utoaji wa kafara za watu umekuwapo enzi na enzi Afrika katika jamii mbalimbali. Kafara ya uhai wa mtu ni ya kiwango cha juu unachoweza kutoa katika utoaji kafara. Waulize wafanya biashara waliotajirika kwa ndondocha watakwambia.

Nimewahi kuhadithiwa kuwa hata wale masultani wakubwa walipofariki dunia walizikwa na mabinti vigoli kadhaa wakiwa hai, kutegemeana na ukuu wa sultani. Wapo waliozikwa na zaidi ya vigoli 20. Kazi yao kule kaburini ni kumpakata sultani.

Usidhani makafara ya kuua watu yameisha Afrika. Pia, sizungumzii hizi kafara ya mtu moja, nazungumzi kafara za halaiki.

Makafara ya halaiki ya binadamu yanaendelea katika bara la Afrika ila kwa mtindo tofauti na kisasa zaidi.

Kama siyo kafara, lugha gani nyingine unaweza kuelezea mauaji ya raia yanayofanyika sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, yaliyofanyika Burundi, Ethiopia, Zimbabwe, Uganda na nchi nyingine mbalimbali za Afrika, yanayotokana na watawala kutaka kubaki madarakani zaidi ya kipindi ambacho Mungu aliwakadiria?

Pale Congo kafara lineanza. Jumatano wiki hii katika Jiji la Kinshasa, ambapo watu 26 waliuawa na vikosi vya usalama. Kosa lao? Waliandamana kushinikiza Rais Joseph Kabila aachie madaraka baada ya muda wake kwisha kwa mujibu wa katiba. Kabila ametawala nchi hiyo tangu mwaka 2001 baba yake alipouawa.

Kabila anataka kuendelea na madaraka. Ili aendelee ameamua atoe kafara raia wa Congo. Nakuhakikishia kuwa huo ni mwanzo tu, watakufa wengi zaidi, watajeruhiwa na watafanywa wawe wakimbizi.

Huku nchi hiyo ikiwa imedumu katika hali ya vita tangu mwaka 1996, bila shaka mgogoro huu mpya utaongeza zaidi waasi na kutanua eneo la uasi na kufutilia mbali matumaini ya kupatikana kwa amani ya kudumu.

Kabla ya kafara la Congo, mwaka jana na mwanzoni mwaka huu kulifanyika kafara kubwa Burundi kumuwezesha Rais Pierre Nkurunziza kuimarisha nguvu zake za kisiasa ili aendelee kutawala zadi ya vipindi viwili alivyostahili kikatiba.

Katika kafara la Burundi, mamia ya watu waliuawa baada ya uchaguzi uliosusiwa na vyama vikuu vya upinzani. Watu waliokuwa wanataka mabadiliko waliingia mitaani kumpinga Nkurunziza, naye akapeleka majeshi kuwasalimia.

Hali huko Zimbabwe

Kule Zimbabwe, Rais Robert Mugabe amekuwa akiendelea na kafara la kuua watu kwa muda mrefu ili azidi kudumu madarakani. Akiwa na miaka 92, hamu yake ya kutawala haijaisha. Hataki hata kurithisha mwanawe! Kufanikisha hilo, Mugabe ametoa kafara maisha ya Wazimbabwe wengi.

Licha ya watu wanaouawa katika mapambano na vyombo vya dola wakipinga utawala wa Mugabe, wapo wengi wanaokufa taratibu kwa sababu ya madhara ya vikwazo vya kiuchumi ambavyo nchi hiyo imewekewa na Marekani na Jumuiya ya Ulaya. Uchumi umevurugika kabisa. Hamu ya kudumu madarakani milele imejisimika katika vinasaba vya viongozi wa kiafrika, na wananchi wa nchi Afrika wanalipia gharama kubwa, ikiwemo kupitia maisha yao yanayotolewa kafara kukidhi matakwa binafsi ya viongozi.

Kule Gambia Rais wa nchi hiyo, Yahya Jammer anakataa kushindwa katika uchaguzi wa kidemokrasia na kukimbilia mahakamani kuiomba ifute matokeo.

Wote tunajua mahakama za Afrika haziaminiki sana kwenye kesi za kisiasa ambazo watawala wana masilahi nazo.

Wananchi hawawezi kuielewa mahakama ikifuta matokeo na kuna uwezekano mkubwa wa kutokea machafuko au tuite kafara jingine la binadamu ambalo kiongozi wa kiafrika anaelekea kutaka kutoa ili kujiimarisha katika utawala.

Jammer, awali, aliushangaza ulimwengu alipotangaza kukubali matokeo na hata kumpigia simu mpinzani wake, Adama Barrow, kumpongeza katika tukio lililorushwa moja kwa moja na televisheni za taifa hilo.

Ilikuwa habari kubwa duniani kwa sababu huenda ingekuwa ni mara ya kwanza kwa rais aliyekuwepo madarakani siyo tu kukubali matokeo ya kushindwa kiunyenyekevu, lakini pia kumpigia mpinzani wake kumpongeza. Siku kadhaa baadaye, Jammer amegeuka na anayakataa matokeo viongozi wenzake wa nchi za Afrika Magharibi hawamuelewi na jumuiya ya kimataifa nayo imekasirishwa.

Uchaguzi Mkuu Kenya

Kenya wanafanya uchaguzi wao mwakani na kuna kila dalili za fujo kutokea nchini humo. Dalili kubwa za uwezekano wa kutokea fujo ni pande kuu za kisiasa kutokubaliana juu ya mchakato wa uchaguzi. Muungano wa vyama vya upinzani umeanza kupata wasiwasi mwingi juu ya uhalali wa kura ya mwakani.

Wasiwasi mkubwa umeibuka baada ya wabunge wa Muungano wa Jubilee (sasa ni chama) walipotumia wingi wao kupitisha uamuzi wa kuruhusu kura kuhesabiwa kwa mkono, kama mfumo wa kielektroniki wa kuhesabia ukifeli.

Cord, wakikumbuka uzoefu wa mwaka 2013, wanaona hii ni janja ya Jubilee ya kutaka kuiba kura. Odinga wa CORD mwaka 2013 alimtuhumu Rais Kenyatta aliyewakilisha muungano wa Jubilee kuwa aliiba kura kwa msaada wa Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (IEBC), baada ya mfumo wa kielectroniki kufeli na kuamuliwa kura zihesabiwe kwa mkono.

Cord tayari wameitisha maandamano makubwa Januari 4 ya kupinga mabadiliko hayo. Ikumbukwe kuwa Cord walishawahi kupata mafanikio makubwa katika maandamano ya Mei na Juni yaliyolazimisha wajumbe wa Tume ya Uchaguzi kujiuzulu.

Pia kumetajwa uwezekano wa upinzani kususia uchaguzi, ingawa kiongozi mmoja wa Jubilee wa Aden Duale, amemwambia Raila Odinga kuwa vitisho vyake havisaidii kwa sababu sheria ya Kenya haisemi kuwa lazima awe mgombea ili uchaguzi uweze kufanyika.

Haya ndiyo makafara ya kiafrika yaliyokuwapo enzi hizo na yanayoendelea kufanyika. Makafara ya binadamu ili watawala waendelee kubaki madarakani na himaya zao ziimarike, hata wawarithishe jamaa zao.

Afrika ni bara la habari mbaya tu kisiasa. Ikitoka hii yaja nyingine. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hali mbaya ilikuwa Burundi, ikaja Kongo, sasa ni Gambia na Kenya ipo njiani. Hii haina maana kuwa wengine ambao nchi zetu hazigongi vichwa vya habari, tumesalimika. Nasi tuna matatatizo yetu lukuki.

Katika baadhi ya hizo kama Sudan ya Kusini, Somalia, Ethiopia na Libya migogoro, mauaji na vita imekuwa ni njia ya maisha. Baadhi ya nchi hizi kama Tanzania hususan Zanzibar na Uganda, Rwanda migogoro inafukuta chini kwa chini. Nchi zinazoonekana zimetulia, kwa mfano Nigeria na Afrika Kusini, zinawindwa na ufisadi wa hali ya juu.

Katika migogoro yote iliyowahi kuripotiwa, jambo moja lipo wazi. Watawala hutumia hisia za kidini, ukabila kuhakikisha wanagawanya watu. Matokeo yake unaona watu wanapambana wenyewe kwe wenyewe, tayari kupoteza hata maisha kwa ajili ya kabila au dini yake, lakini kumbe mwisho wanaofaidika kidhahiri kwa maana maisha kupata maisha bora, ni wachache tu.

Tunapoingia mwaka 2017, Afrika ijiulize maswali magumu. Hali hii itaendelea mpaka lini? Lini tutaanza kutekeleza demokrasia na utawala bora na kuacha ujanja ujanja wa kuimba nadharia hizo bila kuziamini kwa dhati.

Ni kwa kuamini kwa dhati katika demokrasia na utawala bora ndiyo tutapata mafanikio ya kudumu. Lini tutaacha tamaa ya kutawala milele ili makafara ya wanadamu yaishe?

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kwa baruapepe: njonjo.kweja@gmail.com na maoni@mwananchi.co.tz

0 Comments