Kwa ufupi
Hoja kwamba kuna walimu waliofeli kidato cha nne wamekuwa wakijiunga na taaluma ya ualimu imekuwa inatolewa mara kwa mara katika nchi hii. Na hoja hiyo imekuwa mojawapo ya sababu ya kuhalalisha kushuka kwa ubora wa elimu yetu.
Ukiachilia mbali hilo la daraja la nne, inabidi kuzingatia elimu ya ualimu inavyotolewa au jinsi walimu wanavyoandaliwa.
Mtu anayesomea ualimu hasa wa shule za msingi na sekondari hufundishwa mbinu na njia za kumfundisha mwanafunzi. Mbinu na njia hizi huenda sambamba na matumizi ya zana za kufundishia na kujifunzia, vitabu vya kiada, ziada na rejea.
Kwa hiyo, ufaulu hata uwe wa daraja la kwanza, lazima mtu afundishwe ualimu ili awe mwalimu.
Kwenye ualimu tunasema hata mitihani siyo kipimo kizuri cha kupima maarifa ya mwanafunzi, hasa pale mwanafunzi wa msingi au sekondari anasoma mambo maarifa mengi kwa miaka saba au minne kisha anakuja kufanya mtihani kwa saa mbili hadi tatu.
Hata hivyo, kwa mazingira ya shule zetu zisizo na walimu wa kutosha na mazingira bora, hatuwatendei haki wahitimu wenye ufaulu wa daraja la nne tunapowazomea kwamba wamefeli.
Ni dhahiri mazingira yangeboreshwa wangefaulu kwa daraja bora zaidi.
Hata mwalimu mwenye ufaulu wa daraja la kwanza, asipopata mazingira mazuri shuleni kazi yake haiwezi kuzaa matunda mazuri.
Mtalaa wetu wa elimu msingi kwa mfano; una mahitaji yake kuhusu idadi ya wanafunzi kwa mwalimu mmoja.
Uwiano ni wanafunzi 40 kwa mwalimu mmoja, lakini hali ni tofauti, mwalimu mmoja ana kundi kubwa la wanafunzi.
Pia, mtalaa unahitaji kuwepo na vitabu vya kiada, ziada na rejea. Lakini shule zetu hazina vitabu hata vya rejea ukiachilia hivyo vya ziada na rejea.
Mwalimu anatakiwa aingie darasani akiwa na andalio la somo na zana za kufundishia na kujifunzia. Lakini ni walimu wangapi wanafanya hivyo?
Hapa inatakiwa kufanya utafiti wa kina na siyo kuja majibu ya juu ya kulaumu uwezo wa walimu.
Kama leo walimu wanafanya kazi za kuendesha bodaboda baada ya kazi
zao, hao walimu wataandaa masomo na zana kikamilifu? Walimu hasa wavijijini wana mzigo wa masomo kwa siku.
Ukikagua ratiba utakuta mwalimu amejaa kwenye ratiba saa mbili hadi saa tisa. Kwa mazingira hayo mwalimu ataandaaje somo kikamilifu?
Kwenye uandaaji wa somo na zana za kufundishia na kujifunzia, ndiko mwalimu anachagua mbinu na njia za kumsaidia mwanafunzi kujenga uelewa wa anachojifunza, ndiko kunatoa matokeo chanya ya taaluma ya mwanafunzi.
Je, mazingira yanawabeba walimu kufanya hivyo au yanawakatisha tamaa
Hoja kwamba walimu wanaofundisha watoto wa Taifa hili waliefeli, ni kuendelea kuwadharau na kuwafanya kuwa duni watu waliojitoa kufanya kazi katika mazingira magumu.
Joseph Gatahwa ni mwalimu wa shule ya msingi, aliyesoma ngazi ya cheti daraja A na sasa ana shahada ya sanaa na elimu. 0785909051/0767909055
0 Comments