Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi na Maandalizi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Sofia Ali Rijali
WAZAZI wametakiwa kuendelea kuandikisha watoto wao kujiunga na elimu ya maandalizi ambayo kwa mujibu wa Sera ya Wizara ya Elimu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni ya lazima kwa sasa.
Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi na Maandalizi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Sofia Ali Rijali amesema hayo wakati akizungumza na wazee wa mkoani Kaskazini Unguja.
Alisema Serikali imeifanya elimu ya maandalizi kuwa ya lazima ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wanafunzi watakaojiunga na elimu ya msingi kufanya vizuri katika mitihani yao.
Aliwataka wazazi kuitumia fursa hiyo ya kuwapeleka watoto wao kuanza elimu ya maandalizi ambayo inatolewa bure kwa wanafunzi wote.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa, umeonesha watoto wanaojiunga shule kwa kuanza elimu ya maandalizi wamepata mafanikio makubwa ya kuanza vizuri masomo yao katika elimu ya msingi.
Mapema, Ofisa wa Elimu ya Vyuo vya Madrasa, Amina Salum Halfani alisema watoto watakaoanza elimu ya maandalizi watakuwa wakipata mafunzo ya dini ya Kiislamu ambayo yatawawezesha kujua mambo ya msingi ikiwemo kusoma na kuandika.
0 Comments