ELIMU BORA SHULE ZA UMMA BADO SANA

Kwa ufupi

Mwaka huu wametangaza tarehe ya mwisho ya mwezi Januari, takriban wiki tatu kabla ya tarehe ya mwaka jana. Ukizingatia idadi iliyoongezeka ya watahiniwa na zoezi la kuandaa tathmini, wanastahili pongezi kwa kuwa ufanisi umeonekana mwaka huu.

By Mwananchi

Mwaka huu huu Baraza la Mitihani Taifa (Necta), limewahi zaidi kutangaza matokeo ya kidato cha nne tofauti na mwaka jana walipotangaza Februari 18.

Mwaka huu wametangaza tarehe ya mwisho ya mwezi Januari, takriban wiki tatu kabla ya tarehe ya mwaka jana. Ukizingatia idadi iliyoongezeka ya watahiniwa na zoezi la kuandaa tathmini, wanastahili pongezi kwa kuwa ufanisi umeonekana mwaka huu.

Tofauti na miaka iliyotangulia, safari hii napenda niepuke kufanya tathmini kwa kuangalia zaidi takwimu za wanafunzi, shule na ufaulu. Tathmini hiyo inahitaji muda mrefu wa kuangalia taarifa hizo kwa kina, lakini leo napenda tuangalie kwa nini jinamizi la kufeli linaendelea kuziandama shule za Serikali.

Bahati nzuri safari hii hatujapata mshtuko wa shule kongwe kama ilivyokuwa mwaka jana ambapo shule ya Azania ilikuwa miongoni mwa shule 10 za mwisho katika matokeo ya kidato cha sita.

Hata hivyo, Mkoa wa Dar es Salaam una changamoto bado kwani safari hii umetoa shule sita kati ya shule 10 za mwisho kitaifa. Ingawa wengi huwa tunafikiri kuwa Dar es Salaam ni jiji lenye kila aina ya mafanikio na maisha bora, lakini tukiweka ukweli mbele na ushabiki pembeni, Mkoa wa Dar es Salaam ni mgumu sana kwa ajili ya kupata mafanikio kielimu. Ni mgumu kwa upande wa wanafunzi, walimu na hata mazingira ya kujifunzia.

Ugumu wa kwanza ni kuhusu mazingira ya shule nyingi ni kwamba yametelekezwa hasa shule za kata kwa kuwa wanasiasa hawaoni kama umuhimu wa kusimamia ubora wa shule hizo.

Pia, ni mgumu kwa sababu shule nyingi zimezungukwa na mazingira ambayo si rafiki kwa wanafunzi kusoma na walimu kufundisha kwa mafanikio. Utaona shule imejengwa katika mazingira ya kila aina ya fujo na kiasi kwamba hata walimu hawawezi kudhibiti nidhamu ya wanafunzi.

Pia, Dar es Salaam ni ngumu kwa walimu kwa sababu wengi wanaishi mbali sana na shule wanazofundisha na kutokana na gharama za maisha na ushindani wa maisha.

Aidha, walimu wana shughuli nyingine nyingi nje ya kazi ya ufundishaji ili waweze kufanana na wafanyakazi wengine wenye maisha mazuri.

Mbali na hayo, wanafunzi wengi wanaosoma Dar es Salaam wanatoka nyumbani (day students), hivyo imekuwa changamoto kubwa kwao na kwa walimu katika kusimamia usomaji wao.

Kwa wale wanafunzi wanaotoka katika familia zisizo na msingi bora wa malezi, ni rahisi kwao kujiingiza katika makundi mabaya na hivyo kupoteza kabisa mwelekeo wa masomo. Na kwa Dar es Salaam vishawishi vinavyopoteza mwelekeo wa wanafunzi ni vingi.

Pia, tumeona kuwa kuna dalili nyingi za siasa kuharibu elimu yetu kwa baadhi ya wanasiasa kuwaingilia watendaji wa elimu.

Wanasiasa wengi wamekuwa wakifanya maamuzi ya kuwafurahisha wapigakura bila ya kuwasikiliza wataalamu waliobobea katika masuala ya elimu. Pia, wanasiasa wanapoingilia utendaji wa shule hii inaweza kumaanisha kuwa kuna tatizo la uongozi katika shule husika.

Jambo jingine kubwa linalochangia elimu ya Dar es Salaam kuwa mbaya ni ukosefu wa huduma ya chakula shuleni na mabweni.

Ingekuwa huduma ya chakula inatolewa shuleni au kunakuwapo mabweni, ingekuwa rahisi kwa walimu kuwasimamia wanafunzi kitaaluma kwa sababu wanapata muda mwingi wa kuwa nao.

Nirudi katika shule za umma. Tumekuwa tukizungumza zaidi kuhusu shule za Serikali kwa sababu huko ndiko rasilimali watu kubwa zaidi huandaliwa kwa ajili ya taifa nzima.

Shule za Serikali zilipaswa kuwa kimbilio la wengi na nyenzo muhimu ya kuwaendeleza Watanzania wote bila ya kujali dini, rangi, kabila au tabaka la kiuchumi.

Kwa jumla, yako matatizo kama 20 hivi yanayochangia kwa namna moja au nyingine kuwa na matokeo mabaya katika shule zetu.

Matatizo hayo ni uongozi dhaifu wa shule, ukosefu wa ushirikiano wa wadau wa elimu, yaani walimu, wazazi, wanafunzi na viongozi wa kisiasa, miundombinu duni ya kujifunzia na uwekezaji mdogo katika sekta ya elimu.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa mabweni na chakula kwa wanafunzi, huduma duni kwa wanafunzi wa kike wawapo shuleni, walimu kukosa morali ya kufundisha na ukosefu wa walimu wa kutosha shuleni.

Nyingine ni ukosefu wa maktaba, vitabu na vifaa vya kujifunzia na huduma bora kwa mwalimu awapo shuleni na ushirikiano na viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa. Naamini baadhi watasema kuwa shule binafsi zina walimu bora kuliko shule za Serikali, lakini nitapingana na hoja hii kwa kuwa tumeshuhudia shule binafsi zikiwatumia walimu walewale waliotoka shule za Serikali, lakini kilichopo ni kwamba namna ya kuwatumia ndiyo tofauti.

0 Comments