Noel Shao ni mhitimu wa shahada ya elimu Chuo Kikuu cha Dodoma
Kwa ufupi
Kadhalika, niwapongeze wote waliofanya vyema, ikiwa na pamoja na wale waliochangia matokeo haya mazuri. Pia, niwatie moyo wale ambao matokeo hayakutoka kama walivyotarajia kwa sababu mbalimbali.
By Noel Shao
Nipongeze kazi kubwa ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kwa kutoa matokeo kwa wakati. Hii ni ishara ya usimamizi na utendaji mzuri.
Kadhalika, niwapongeze wote waliofanya vyema, ikiwa na pamoja na wale waliochangia matokeo haya mazuri. Pia, niwatie moyo wale ambao matokeo hayakutoka kama walivyotarajia kwa sababu mbalimbali.
Matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2016, yameleta picha tofauti ambazo tunaweza kuzitumia kupongeza, kurekebisha au kuboresha.
Pamoja na ongezeko la kutoka asilimia 67.53 hadi asilimia 70.9, habari zaidi ni mwendelezo wa shule binafsi kuongoza kufaulisha, huku za umma zikiongoza kufeli. Kwa hiyo zote zinaongoza ila kwa namna tofauti.
Ni takribani miaka mitano mfufulizo shule za umma hasa za vipaji maalumu zimepoteza ile sifa ya ushindani. Kuzidi kuzorota kwa shule za umma, kusiwe na sababu moja inayopambanua sababu za kufeli huko. Kwangu, sababu nazikita kwa wadau wakuu watatu wa elimu nchini.
Wa kwanza ni Serikali na watendaji wake. Hawa ndio watunzi wa sera, mitalaa na wasimamizi mama wa mfumo wa elimu.
Ni wajibu wa Serikali kusimamia utaratibu wa utoaji na upatikanaji wa elimu bora. Serikali chini ya wizara husika lazima wajikite katika kutafiti nini chanzo cha anguko kubwa la elimu hasa katika shule za umma.
Wazingatie kutafuta suluhu ya kudumu ya mwendelezo huu wa matokeo yasiyoridhisha. Watazame ubovu wa mitalaa ambayo achilia mbali upungufu wake, imekuwa ikibadilika kila mara jambo linaloleta usumbufu katika kufundisha na kujifunza.
Suala la kuboreshwa kwa miundombinu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia, maslahi kwa walimu, ni jukumu la Serikali. Je? Serikali imesimama vema katika kutimiza wajibu wake huo, kama jibu ni hapana, hapa ndipo tunapozalisha sababu ya kwanza ya wanafunzi kufeli.
Kundi la pili ni wazazi. Kundi hili kwa upande fulani limejisahau na kuwa chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili na nidhamu za watoto, hivyo Hivyo kusababisha ufanisi wa nidhamu ya shule nayo kushuka.
Kwa kisingizio cha majukumu na kutingwa na shughuli za maisha, wazazi wamesababisha watoto wengi kujitumbukiza katika mambo yaliyo juu ya umri wao. Kwa mfano, wameshindwa kabisa kudhibiti madhara mabaya ya utawandawazi.
Wazazi wamejisahau na wengi wamekimbia majukumu ya malezi; wameamua kuwaachia walimu majukumu ya kulea watoto wao au wafanyakazi wa ndani, wakiwa na imani potofu kuwa jukumu lao ni kulipa ada tu.
Siyo jambo geni kuona muhula mzima mzazi hajafika shuleni kufuatilia maendeleo ya mtoto wake. Na mtoto akirudi nyumbani vivyo hivyo hakuna ufuatiliaji.
Tatu ni walimu, hawa ndio jeshi linalopaswa kuwa katika mstari mnyoofu katika kufikisha gurudumu la elimu. Kuna walimu wengi katika shule za umma wamepoteza ari na hamasa ya kufundisha.
Unajiuliza inakuwaje shule binafsi hazina vyuo vyao vya kuzalisha walimu, lakini zinafaulisha? Tafakuri itakueleza wazi kuwa kuna upungufu sehemu fulani.
Wito wangu, tunaelewa mfumo wa elimu unahitaji marekebisho ili kukidhi mahitaji ya kimaendeleo kwa taifa, ila kwa sasa nahimiza wadau hao watatu wasimame kwenye nafasi zao, ikitokea mmoja anatega tusitegemee mabadiliko.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa nchini. 0769735826
0 Comments