IFM YAOMBA KUWA CHUO KIKUU

SERIKALI imesema imepokea ombi la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) la kutaka kupandishwa hadhi na kuwa Chuo Kikuu, kutokana na kukidhi vigezo. Imeahidi kufanyia kazi ombi hilo kwa kushirikiana na wadau wengine ili kufanikisha jambo hilo, bila kupindisha utaratibu wa serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Dk Anthony Mavunde wakati akizindua Baraza la Tisa la Wafanyakazi la chuo hicho.

"Sishangazwi na ombi lenu la kuwa Chuo Kikuu, nimelichukua na ninaahidi kuwasiliana na wadau wengine wa serikali tunone njia bora ya kuliendeza bila kupindisha taratibu," alisema Mavunde.

Mavunde ametaka Baraza hilo jipya kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanatekeleza mipango waliyojiwekea ambayo inaendana na utekelezaji wa wa mipango ya serikali.

Amesema mabaraza mengi ya wafanyakazi yanaykumbana na changamoto, ikiwemo ya kuikosa kuaminiana kati ya menejimenti na wafanyakazi hatua ambayo husababisha kila pendekezo linalowasilishwa kwenye baraza kukataliwa na wafanyazi.

"Lakini nimeelezwa kuwa kwenu hakuna Tatizo hili, naomba muendelee na kuaminiana katika kusukuma maendeleo ya Chuo na Taifa kwa ujumla," amesema.

Awali, Mkuu wa chuo hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Profesa Taadeo Sata alisema, chuo hicho kwa sasa kinatekeleza mradi wa upanuzi wa chuo hicho katika eneo la Msata, Bagamoyo mkoani Pwani.

Alisema pamoja na kwamba chuo hicho kinatafuta pesa kupitia vyanzo mbalimbali lakini kinahitaji msaada wa serikali ili kukamilisha ujenzi huo.

"Baraza la wafanyakazi wa chuo ni muhimu kwa maendeleo ya chuo chetu. Kwa sasa tumedahili wanafunzi zaidi ya 8,000 katika fani mbalimbali na tuna wahadhiri 152," alisema.

Mwenyekiti wa Baraza la IFM, Letticia Rutashobya alisema chuo hicho kinatekeleza mikakati mbalimbali ya kuoberesha chuo hicho. Waziri Mavunde pia alitembelea eneo litakalojengwa Chuo cha IFM lililopo Msata ambalo lina ukubwa wa ekari 1,500.

0 Comments