TAASISI ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI) ina mpango wa kuzipa uwezo wa utaalam wa madaktari, tiba na baadhi ya vifaa hospitali tano zilizopo Dar es Salaam, Pwani na Morogoro kwenye vitengo vyao vya majeruhi, lengo likiwa ni kurahisisha kupunguza majeruhi wanaowapokea kila siku.
Hospitali hizo ni Amana, Temeke, Mwananyamala, Tumbi na Morogoro ifikapo mwaka mpya wa fedha.
Kaimu Mkurugenzi wa MOI, Dk Othman Kiloloma alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Moi uliofanyika kwenye Ukumbi wa Idd Nyundo wa Manispaa ya Temeke.
Dk Kiloloma alisema watakapoanza utaratibu huo, kwenye vitengo vya majeruhi katika hospitali hizo ambapo wafanyakazi wao watakuwa wanakwenda kwa zamu katika maeneo hayo, anaamini wingi wa majeruhi watakaofikishwa Moi utapungua kwa kuwa hospitali hizo zitakuwa zikifanya huduma kama zao.
Alisema wao watatoa utaalamuna Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), watapeleka vifaa vinavyohitajika.
“Kwa kufanya hivi tunaamini itarahisisha kupunguza majeruhi wanaofika katika taasisi yetu, kwani watahudumiwa huko huko walipo ila wale wenye majeraha makubwa ndio tutakaowapokea,” alieleza.
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye alikuwa mgeni rasmi, Profesa Bakari Lemberiti alisema vikao vya baraza hilo vitatumika kwa namna ya pekee kujadili, mipango, maendeleo, mikakati, matarajio utekelezaji na maazimio ya vikao vilivyopita.
Pia kuweka maazimio mapya na kuzijadili changamoto kwa kina na kutafuta majawabu ya changamoto hizo kama ambavyo wamekuwa wakifanya katika vikao vilivyopita.
0 Comments