MUHIMBILI YAZINDUA ENEO LA WATOTO

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Julieth Magandi akikata utepe kuzindua sehemu ya kuchezea watoto wanaotibiwa Muhimbili. Dk Magandi amezindua sehemu ya kuchezea watoto kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Tiba Muhimbili, Dk Hedwiga Swai na mwakilishi wa Human Welfare Trust, Bi. Veena Jog.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Julieth Magandi akizungumza kabla ya kuzindua sehemu ya watoto kuchezea. Kushoto ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa Benki M, Anil Verma.

Baadhi ya wageni waliofika Muhimbili kushuhudia uzinduzi huo wakimsikiliza mgeni rasmi Dk Magandi.

 Baadhi ya watoto, wauguzi, madaktari na wageni wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Dk Magandi leo.

 Mwakilishi kutoka Human Welfare Trust, Bi. Veena Jog akizungumza kabla ya uzinduzi huo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha akishiriki kuimba na watoto hao leo.

Watoto wakicheza baada ya sehemu ya kuchezea kuzinduliwa leo katika hospitali hiyo.

……………

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto leo imezindua sehemu ya kuchezea watoto wanaolazwa  na wale wanaofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kupatiwa matibabu mbalimbali.

Sehemu ya kuchezea watoto imezinduliwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa hospitali hiyo, Dk Julieth Magandi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya.

Akizindua sehemu ya kuchezea watoto, Dk Magandi amesema kuwapo kwa sehemu ya kuchezea kutaongeza chachu ya watoto kuacha kuogopa hospitali kwani watavutiwa na kutambua kwamba wapo katika mazingira salama na rafiki wakati wakipatiwa huduma za matibabu.

“Nawapongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili licha ya kufungua sehemu hii ya michezo leo bado ndani ya jengo mmeweka vivutio vingi kwenye kuta zote za jengo la watoto ili kuhakikisha watoto wanafurahi,” amesema Dk Magandi.

Dk Magandi amesema kuwa sehemu hiyo ya michezo ambako pamefungwa vifaa vya kisasa vya kuchezea itawasaidia watoto wanaokaa muda mrefu hospitalini kuanzia mwezi mmoja hadi mwaka mmoja kupata faraja.

 “Nina imani kuwa sehemu hii itawapa uhuru wa kucheza kwa nafasi na usalama zaidi ukilinganisha na hali ilivyokuwa awali.  Ni kweli ndani ya jengo  kuna michoro ya wanyama mbalimbali na katuni zinazotoa taswira rafiki kwa watoto na kuondoa mawazo ya kwamba hospitali ni sehemu ya maumivu muda wote, lakini kuongezeka kwa sehemu hii ya michezo itachochea zaidi hali ya watoto kupenda kutibiwa na kujisikia huru zaidi,” amesema.

Pia, Dk Magandi amewashukuru Human Welfare Trust Fund kwa kujenga sehemu ya kuchezea watoto kwani wameonyesha wanawajali watoto wetu.

Naye Mkurugenzi wa Tiba katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Hedwiga Swai akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru amesema kwamba watoto wanaolazwa katika Jengo la Watoto ni wale wanaohitaji tiba za upasuaji, wenye majeraha ya moto, utapiamlo, matatizo ya moyo, wenye matatizo ya mishipa ya fahamu, figo, magonjwa ya tezi na kisukari, magonjwa ya mfumo wa damu, macho na watoto wanaohitaji ushauri wa lishe bora.

“Sehemu hii ya michezo itatumika kwa watoto wanaokuja kliniki kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, wale wanaofatiliwa maendeleo yao baada ya kupata nafuu na wale wanaopata ruhusa ya kurudi nyumbani na watoto waliolazwa wodini,” amesema Dk Swai.

0 Comments