KATIKA kuhakikisha kuna sheria, viwango na miongozo ambayo inatengeneza mazingira mazuri ya kupanua na kuboresha utoaji wa elimu nchini, Tume ya Kikristo ya Kuhudumia Jamii (CSSC) imeanzisha mazungumzo na serikali ya kupandisha alama ya wastani ya ufaulu wa kidato cha pili kutoka asilimia 30 iliyopo sasa hadi asilimia 40.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo, Peter Maduki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 25 ya tume hiyo, yatakayofanyika Februari 21 na 22, mwaka huu.
Maduki alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona kiwango kilichopo sasa ni kidogo na kwa kufanya hivyo kutasaidia kuboresha elimu na kuwa sawa na alama za wastani za ufaulu katika ngazi nyingine za elimu.
“Ufaulu kwa ngazi nyingine za elimu unataka ufaulu kwa wastani wa asilimia 40 hivyo ni bora tukaanza kujenga msingi huo huku chini ili kuwafanya wanafunzi hawa kuwa bora mbeleni,” alieleza Maduki.
Tume ya Kikristo ya Kuhudumia Jamii (CSSC) ni chombo kilichoundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa lengo la kuratibu kusimamia huduma za kijamii zitolewazo na taasisi za makanisa hususani za elimu na afya nchini.
Pia alisema ili kuboresha sekta ya elimu, makanisa bado yanaendelea kuanzisha na kuendesha taasisi za elimu katika ngazi mbalimbali na hadi mwishoni wa mwaka jana, makanisa yalikuwa yanamiliki taasisi za elimu zipatazo 1,006.
Aliongeza kuwa katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya afya unapatikana kwa uhakika kupitia tume na taasisi za makanisa za utoaji wa huduma za afya zipatazo 900 ambazo ni pamoja na hospitali 102, vituo vya afya 102, zahanati 696.
Pia alizungumzia changamoto zinazoikabili tume hiyo ni pamoja na uelewa mdogo wa baadhi ya wamiliki na watendaji wa taasisi za makanisa, baadhi ya watendaji serikalini na wanasiasa juu ya sera, sheria na miongozo ya utoaji wa huduma ya elimu na afya baadhi yao kukosa utashi wa kutekeleza sera, sheria na miongozo.
Changamoto nyingine ni upungufu wa rasilimali watu.
0 Comments