Frank Chalamila
Kwa ufupi
Naandika haya, nikisadifu matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka hivi karibuni na jitihada za wadau wa elimu katika kuinua taaluma nchini.Natambua wapo wanaofanya tathmini ya wapi tumetoka, tulipo, na wapi tunakwenda kama taifa, na kama wadau wote kwa pamoja tunayatambua na kuyaishi majukumu yetu bila kusukumwa na tena kwa usahihi kabisa.
By Frank Chalamila
Ukiusikiliza kwa umakini wimbo huu usemao “mwenda pole hajikwai, akijikwaa haumii, akiumia huumia kidogo tu,” utagundua kuwa kila mwenye uthubutu chanya katika jambo fulani japo atapita katika magumu ya hapa na pale lakini mwisho wake hufanikiwa.
Naandika haya, nikisadifu matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka hivi karibuni na jitihada za wadau wa elimu katika kuinua taaluma nchini.
Natambua wapo wanaofanya tathmini ya wapi tumetoka, tulipo, na wapi tunakwenda kama taifa, na kama wadau wote kwa pamoja tunayatambua na kuyaishi majukumu yetu bila kusukumwa na tena kwa usahihi kabisa.
Naamini pakiwapo mshikamano wa mizania sawa kwa wadau wote bila kujali nani ni nani, ni dhahiri itakuwa rahisi kubaini upungufu wetu na hivyo kufanya maboresho ya safari ya elimu.
Mwandishi ‘Malala Yousafzal’ anaandika katika kitabu chake akisema “Kitabu kimoja, kalamu moja, mwanafunzi mmoja, na mwalimu mmoja watabadilisha ulimwengu”
Anasisitiza wadau wote kuinua taaluma, kwamba kama mzazi au mlezi akitimiza wajibu wake, mwalimu akitimiza wajibu wake, mwanafunzi akatimiza wajibu wake, Serikali ikatimiza wajibu wake, lazima mafanikio chanya yawepo.
Ninachokiona hivi sasa hasa baada ya matokeo haya ni kwamba kuna shule zilizofanya vizuri kama ilivyo ada yao na zipo shule zilizofanya vibaya kama ilivyo mipango yao ya ovyo zikiwamo za vipaji maalumu.
Niliwahi kuandika makala mwaka jana kuhoji shule za vipaji maalumu kupwaya katika matokeo ya ufaulu wa mitihani ya taifa, bado mwaka huu hakuna shule ya vipaji maalumu hata moja iliyoweza kuingia walau kumi bora. Zipo shule ambazo matokeo yake ya ufaulu kwa daraja la sifuri yameongezeka kwa kasi, na wala hatuoni jitihada mbadala zikifanywa na uongozi wa shule, wazazi na wadau wengine.
Ukweli ni kwamba viongozi wa elimu na hasa wakuu wa shule, maofisa elimu na waratibu katika ngazi husika, wanakwama kutanabahisha wapi wamekosea na nini cha kufanya katika kuinua taaluma katika himaya zao.
Sijaona mikakati mbadala na chanya ya kuboresha taaluma. Serikali imeamua kugharimia elimu, hivi sasa madawati na ukosefu wa ada siyo matatizo tena, lakini.
Kwa nini maofisa elimu na wakuu wa shule wasijikite katika kutumia taaluma zao kuboresha taaluma kwa kuwa wabunifu?
Viongozi hawa wamekuwa wagumu hata kujifunza mapya japo yana tija, huioni mikakati mipya ikiratibiwa na watu hawa hata kama watapokea ushauri bora. Wao kazi yao kuu ni kuilamu Serikali tu. Shuleni wakuu wa shule kazi yao kubwa ni kuunda makundi yakiwamo ya majungu ya mwalimu nani anafanya nini. Hawana makundi ya kuratibu mikakati thabiti ya kuinua taaluma katika shule zao.
Tathmini yangu fupi inaonyesha kuwa kwa shule ambazo zina vituo vya kufanyia mitihani ya “watahiniwa wa kujitegemea’, nguvu kubwa ya uongozi wa shule ipo katika eneo hilo kwani ni mahali wakuu wa shule wanapata fedha za moja kwa moja.
Naamini wakuu wa shule wana nafasi kubwa ya kubadili hali ya mambo katika shule zao hasa kama wataruhusu mawazo na ushauri kutoka kwa wengine.
Umimi na makundi kamwe hayajengi, ni heri basi makundi hayo yangekuwa ya kuleta maendeleo shuleni. Ni makundi ya majungu na kulinda uluwa wa wakuu pekee. Hatutofika.
0 Comments