HALMASHAURI YA MOROGORO YATAKA WANAFUNZI WAPATE CHAKULA SHULENI


MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo, amewataka madiwani wa Halmashauri hiyo kushirikiana na wananchi kuweka utaratibu wa wanafunzi kupata chakula shuleni.

Alisema hivi karibuni kuwa hiyo itawawezesha wanafunzi hao hasa wa shule za msingi, kupenda kuhudhuria masomoni na hivyo, kupunguza utoro.

Kingo alikuwa katika Kata ya Mvuha, wilayani humo alipokuwa mgeni rasmi katika sherehe zilizoandaliwa na Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali la Right To Play – Tanzania.

Shirika hilo linafadhili mradi wa elimu wa kujenga uwezo wa kusoma wanafunzi katika shule za msingi 15 sita zikiwa za Manispaa ya Morogoro na tisa kutoka Hamashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Alisema njia mojawapo ya kumwezesha mtoto kuwa na akili darasani ni upatikanaji wa chakula shuleni kwa kuwa mtoto mwenye njaa hawezi kumudu vema masomo.

Kutokana na changamoto hiyo, aliagiza kila diwani ahamasishe wananachi wakiwemo wazazi na walezi kutoa chakula kwa ajili ya mlo wa wanafunzi shuleni.

“Halmashauri hii ina utajiri wa mazao ya chakula na si vibaya sisi madiwani kwenye kila kata tunajitokeza kuwahamaisha wazazi, walezi na wananchi wachangie chakula cha watoto shuleni, ili watoto wetu wapate kusoma vizuri... Wengi wanatoka mbali na shule,” alisema.

Aliwahimiza wazazi na walezi kuachana na mila potofu zinazowabagua watoto wa kike na kuwakwamisha malengo yao kielimu.

Naye Mratibu wa Mkoa wa Morogoro wa Right To Play –Tanzania, Mourine Msangi alisema, shirika linashirikiana na serikali kuboresha mtaala kwa kuhusisha Mamkala ya Elimu Tanzania unaolenga shule za msingi kujenga ubora wa elimu kupitia michezo ikiwa na kuboresha elimu ya awali ambayo ni msingi ya elimu nchini.

0 Comments