MRADI KUKABILI MABADILIKO YA TABIANCHI KUNUFAISHA SHULE

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake, ofisi yake imeandaa mradi utakaonufaisha shule za msingi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Akiwa wilayani hapa, January alisema moja ya changamoto za Wilaya ya Bagamoyo ni ukame unaotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, uliosababisha kupanda kwa kina cha bahari na kusababisha visima vilivyochimbwa pembeni mwa miji na fukwe za bahari kufukiwa na maji na chumvi.
“Ofisi ya Makamu ya Rais imeamua kuisaidia Wilaya ya Bagamoyo kuchimba visima kumi na saba virefu kwenye maeneo ambayo yameathirika na kupanda kwa kina cha maji na maeneo yenye ukame mkubwa,” alibainisha January.

Takribani kila kisima kitagharimu Sh milioni 50 na Ofisi ya Makamu wa Rais pia itaandaa mfumo wa kuvuna maji katika shule tano mradi utakao gharimu takribani Sh milioni 170.
Katika hatua nyingine, alitembelea Kiwanda cha Sea Salt kilichopo Saadani kuona namna kiwanda kinavyofanya kazi kwa kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.

Juzi jioni, aliwasili mkoani Tanga kujionea hali ya mazingira na changamoto za uhifadhi, akitembelea Wilaya ya Pangani na kukagua mradi wa ujenzi wa Ukuta wa Pangani.

Alimtaka mkandarasi anayejenga ukuta wa mto Pangani Kampuni ya Dezo Civil Construction Limited kukamilisha ujenzi wa ukuta kwa kipindi cha miezi 10 kama mkataba unavyoonesha na kuzingatia ubora.

Ujenzi huo wa sehemu ya ufukwe wa kaskazini ambao una urefu wa mita 950 ambazo kati yake mita 550 zipo katika ujenzi wa awali, utagharimu Sh bilioni 2.4.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdalah alimuomba Waziri kutuma timu ya wataalamu kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kwa fukwe pekee iliyoko katika maeneo ya Tanga DECO ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na haipo katika bajeti kwa mwaka huu wa fedha.

0 Comments