Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lenye dhamana ya kuratibu ukuzaji na uendelezaji wa sekta ya Sanaa nchini litatoa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini waliofanya vizuri kitaifa katika masomo ya Sanaa za Muziki, Ufundi na Maonyesho kwenye matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika mwezi Oktoba,2016 na matokeo yake kutoka hivi karibuni. Aidha, sambamba na kutunuku vyeti na Zawadi za fedha taslimu kwa wanafunzi hao BASATA litatambua mchango wa walimu wa masomo husika na shule zilizofanya vizuri katika mchepuo wa Sanaa.
Hafla hiyo ambayo itawakutanisha wanafunzi hao, walimu wao pamoja na wadau mbalimbali wa Sanaa itafanyika siku ya Jumatatu tarehe 27/03/2017 saa 4:00 asubuhi katika Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Ili kutambua,kuibua na kukuza vipaji vya Sanaa kutoka ngazi za chini na kuamsha ari ya masomo ya mchepuo wa Sanaa katika mitaala yetu ya elimu sambamba na kujenga weledi katika tasnia ya Sanaa kwa ujumla wake Baraza limeamua kurejesha programu hii ya utoaji wa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari kila mwaka ambao wanashika nafasi za juu kitaifa katika masomo ya sanaa husasan Sanaa za Ufundi, Maonyesho na Muziki
Itakumbukwa kuwa BASATA limekuwa na mwendelezo wa programu mbalimbali za Sanaa kwa watoto zilizoanza tangu miaka ya 1980 ambazo zimepata kuibua na kukuza vipaji vya wasanii. BASATA linachukua fursa hii kuwaalika wananchi na wadau wote wa sanaa kufika kwa wingi kushuhudia utoaji wa tuzo hizi.
Sanaa ni kazi, tuipende, tuikuze na kuithamini
Godfrey Mngereza, Katibu MTENDAJI. 23 MACHI, 2017
0 Comments