Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema umefika wakati vyombo vya habari vipewe ulinzi, na kuhakikisha haviingiliwi na mtu wala mamlaka yoyote kwa manufaa binafsi.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba alisema kuwa vyombo vya habari vipo na vinaongozwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016, hivyo kwa namna yoyote iwayo, vinapaswa kuheshimika na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, badala ya kuingiliwa.
Alisisitiza kuwa matumizi yoyote ya vyombo vya dola katika kudidimiza uhuru wa vyombo vya habari ni jambo linalopaswa kukemewa vikali kwani ni uvunjaji misingi iliyowekwa na Katiba ya Mwaka 1977 Ibara ya 18.
Dk Bisimba aliitaka Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kurejea mapendekezo ya wadau juu ya sheria kandamizi kwa uhuru wa habari ili kutoa ulinzi kwa vyombo vya habari na wanahabari, badala ya kuibuka katika tukio moja.
0 Comments