Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo amekutana na kufanya mazungumzo na washirika wa Maendeleo kutoka nchini Uingereza (DFID) ambapo Kwa pamoja wamekubaliana kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ikiwa ni pamoja na kuboresha Miundombinu katika sekta ya Elimu.
Waziri Ndalichako amefanya mazungumzo hayo mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine waziri amesisitizia zaidi suala la kuboreshwa Kwa mazingira ya kujifunzia Kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, kusisistiza kuwa eneo hilo linahitaji kuwekewa Nguvu zaidi.
Waziri amewaeleza washirika hao wa maendeleo kuwa zipo changamoto katika shule za wanafunzi wenye mahitaji maalumu, hivyo ili kuwawezesha wanafunzi hao lazima miundombinu iwe rafiki ambayo itawasaidia kufanya vizuri katika masomo yao.
Waziri pia amezungumzia suala la ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi wa kike, hususan kwa wale wanaoishi vijijini.Amesema wanafunzi wa kike wanapata changamoto ya mimba za utotoni kutoka na baadhi ya shule kukosa mabweni na hivyo wanafunzi hao wakike kuingia kwenye vishawishi.
Pamoja na mambo mengine waziri Ndalichako pia ameelezea baadhi ya changamoto ya kuwepo Kwa Elimu bila malipo kuwa ni pamoja na uhaba wa vyumba vya madarasa, uhaba wa matundu ya vyoo, uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi.
0 Comments