SHULE 120 ZINAZOFANYA VIZURI KUPATA UFADHILI WA BENKI YA DUNIA

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako

KWA miaka mitatu kuanzia mwaka 2014 hadi 2016, Benki ya Dunia imetoa ufadhili wa elimu kwa shule za msingi 120 zinazofanya vizuri kitaaluma kutokana na mpango uliopo wa ‘Lipa Kulingana na Matokeo’ ambao umeangalia matokeo ya darasa la nne na la saba ya mtihani wa Taifa kwa shule hizo zilizopo Dar es Salaam.

Aidha, ufadhili huo umetolewa kwa vyuo vikuu nchini katika masuala ya mafunzo, rasilimali watu na miundombinu.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akimkaribisha Rais wa benki hiyo, Dk Jim Yong Kim alipotembelea mojawapo wa shule hizo za msingi ambayo ni Zanaki katika Manispaa ya Ilala.

Alisema pia wamewekeana makubaliano na benki hiyo ya kuendelea kujenga madarasa ambapo dola za Marekani milioni 75 (sh bilioni 157.5 ) zimetengwa na benki hiyo kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri zaidi ya kujifunzia pamoja na elimu maalumu.

“Benki ya Dunia inasaidia sana elimu, shule nyingi zimejengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na vyuo vikuu kwenye miundombinu pamoja na rasilimali watu,” alieleza.

Naye Rais wa Benki ya Dunia anayezuru nchini kwa ziara ya siku tatu, Dk Kim alisema anafurahishwa na matokeo ya shule hiyo ya Zanaki, hivyo ameahidi kuendelea kuisaidia, lakini pia ameishauri serikali kuwekeza zaidi kwenye elimu.

Alisisitiza kuwa ili nchi iwe na uchumi endelevu ni vema ikawekeza kwenye elimu kwa kuwa elimu inatoa ujuzi mbalimbali.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jackson Kashaija alisema Zanaki inayo furaha kuwa miongoni mwa shule 120 zinazonufaika na ufadhili huo unaotolewa na Benki ya Dunia wa programu ya matokeo mazuri ambayo inaongeza bidii katika masomo.

Kashaija alisema pamoja na msaada huo bado wana changamoto kwa kuwa kwenye madarasa kuna mlundikano wa wanafunzi, na kwamba miundombinu iliyojengwa awali ilikuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 322, lakini sasa kutokana na ufaulu wanafunzi wameongezeka hadi kufikia 1,100.

0 Comments