Kwa ufupi
Pia huweza kuisaidia jamii yake kutatua changamoto za kimaisha. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kuwa mtu aliyepata elimu stahiki ni kiongozi katika jamii yake.Umahiri wa elimu ya mtu hujidhihirisha kutokana na fikra pamoja na matendo yake. Ili tujenge taifa lenye wananchi wenye uwezo wa kutatua changamoto zao za kimaisha, hatuna budi kujenga utamaduni wa kusoma vitabu.
Elimu ni nyenzo muhimu katika maisha ya binadamu.Mtu aliyepata elimu stahiki huwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Pia huweza kuisaidia jamii yake kutatua changamoto za kimaisha. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kuwa mtu aliyepata elimu stahiki ni kiongozi katika jamii yake.
Umahiri wa elimu ya mtu hujidhihirisha kutokana na fikra pamoja na matendo yake. Ili tujenge taifa lenye wananchi wenye uwezo wa kutatua changamoto zao za kimaisha, hatuna budi kujenga utamaduni wa kusoma vitabu.
Chanzo kikuu cha maarifa yote ambayo binadamu huyapata, hutoka kwenye vitabu. Vitabu ni njia nzuri ya kutunza maarifa na historia ya mambo ya kale, mambo ya sasa na mambo yajayo.
Mtu mwenye utamaduni wa kusoma vitabu huwa na uwezo mzuri wa kufikiri, kuchanganua mambo, kutafuta njia sahihi za kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha, kuifahamu lugha na kuitumia kwa ufasaha pamoja na kuona fursa mbalimbali na kuzifanyia kazi.
Mfano mzuri tunauona kwa Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa msomaji mzuri wa vitabu. Sifa nyingi alizokuwa nazo mwalimu ikiwa ni pamoja na kuwa na uelewa mpana wa mambo mbalimbali, zilichangiwa na maarifa aliyoyapata kutoka kwenye vitabu alivyovisoma.
Pia, Nyerere aliandika vitabu vinavyohusu masuala mbalimbali ya kijamii na vimekuwa vikipendwa na watu wengi ndani na nje ya nchi yetu.
Mfano mwingine ni wa aliyekuwa rais wa Marekani Barack Obama ambaye anasifika kuwa ni miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa duniani.
Uwezo wake wa kupambanua mambo umetokana na utamaduni wa kusoma vitabu mbalimbali. Vitabu pia vimemfanya awe mwandishi mahiri wa vitabu.
Mataifa ya Magharibi yameendelea kutokana na utamaduni wa kusoma vitabu ambavyo huwapatia maarifa yanayowafanya wawe wabunifu wa mambo mbalimbali yenye manufaa kwa jamii yao na ulimwengu kwa jumla.
Kwa bahati mbaya, Watanzania hatuna utamaduni wa kusoma vitabu, kutokana na msingi mbovu tuliojengewa tangu tukiwa bado wadogo. Kuna utani mmoja ambao watu hutaniana kuwa, “ukitaka kumnyima Mtanzania zawadi iweke kwenye kitabu”.
Haishangazi kukuta mwanafunzi wa chuo kikuu hana kitabu hata kimoja cha ziada alichonunua, mbali na vitabu anavyotumia darasani.
Utafiti unaonyesha kuwa, mtoto aliyejengewa utamaduni wa kusoma vitabu hasa vya hadithi tangu akiwa mdogo, huwa mdadisi, hujua mambo mengi na hufanya vizuri katika mitihani yake darasani.
Hii hutokana na kuwa na maarifa mengi anayoyapata kutoka kwenye vitabu anavyosoma.
Ili kuwajengea watoto wetu utamaduni wa kusoma vitabu, wazazi wanapaswa wajenge tabia ya kuwasimulia hadithi za kuvutia tangu wakiwa wadogo ili wawe na shauku ya kupenda kufuatilia hadithi na pindi wanapojua kusoma, wazazi wawanunulie vitabu vya hadithi ili wavisome badala ya kuwasimulia hadithi.
Vitabu vya hadithi vitawafanya watoto wapende kusoma vitabu vyote hata vile vya kiada ambavyo huvitumia darasani. Pia vitabu vitawafanya wawe wadadisi wa mambo na hivyo kupata maarifa mengi yatakayowawezesha kufanya vizuri katika mitihani yao.
Tukumbuke kuwa mtoto anapozaliwa ubongo wake huwa tupu, ni jukumu la mzazi au mlezi kuchagua vitu vya kuujaza ubongo wa mtoto wake.
Ukitaka mtoto wako awe na akili, unapaswa uanze kumjenga tangu akiwa mdogo.
0 Comments