Viongozi wa TAS wakiondoka katika kanisa la KKKT Usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria.
Chama cha watu wenye ualbino nchini (Tanzania Albinism Society-TAS) kimeanza kampeni ya kutoa elimu kuhusu masuala ya ualbino katika nyumba za ibada ambapo leo viongozi wa chama hicho taifa wametoa elimu katika kanisa la KKKT Usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria lililopo mjini Shinyanga.
Viongozi hao wakiongozwa na Afisa Mahusiano na Habari kutoka TAS ,Josephat Torner wametoa elimu kuhusu mambo ya ualbino kanisani hapo wakati wa ibada ya Jumapili leo Machi 26,2017.
Akizungumza kanisani hapo Torner alisema kampeni hiyo inalenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya ualbino kwa viongozi wa dini na waumini wao na wanaendelea pia kutoa elimu hiyo kwa makundi mengine ya watu katika jamii wakiwemo waganga wa kienyeji.
“Tumeona vita hii tunayopambana nayo bila kumjua hasa adui ni nani,ni vyema elimu iwafikie watu wengi zaidi na tunaamini kupitia nyumba za ibada jamii itakuwa na uelewa wa kutosha juu ya masuala ya ualbino ili kukabiliana na tatizo la mauaji ya watu wenye ualbino na hata vitendo vya kufukua makaburi ya watu wenye ualbino vinavyoendelea kujitokeza nchini”,alieleza Torner.
Alisema bado watu wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu masuala ya ualbino hali inayosababisha kuongezeka kwa unyanyapaa ambapo sasa hata wamiliki wa nyumba za kupanga wanawanyima vyumba watu wenye ualbino wakihofia kupata matatizo.
“Nyumba za ibada zina watu wengi,tutapita kwenye makanisa na misikiti kutoa elimu hii ili viongozi na waumini waelewe hasa maana ya ualbino ili tuungane pamoja kutokomeza vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino”,aliongeza Torner.
“Kutokana na imani potofu katika jamii watu wenye ualbino wanaishi kwenye vituo maalum,wanaishi kwa hofu kubwa ya kuuawa na sasa kuna baadhi ya watu wameanza kufukua makaburi ya watu wenye ualbino hivyo kunahitajika jitihada zaidi katika kupambana na ukatili huu”,alisema Torner.
Alisema mbali na jitihada zinazofanywa na serikali katika mapambano dhidi ya ukatili huo ni vyema jamii ikatoa ushirikiano katika kupiga vita vitendo hivyo vya kikatili.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa kanisa hilo,Mchungaji Jackson Maganga alisema kanisa hilo lina programu nyingi za kutoa elimu kwa waumini wake juu ya vitendo vya ukatili kwa watu wenye ualbino na kwamba kanisa hilo liko tayari kushirikiana na chama hicho katika mapambano dhidi ya ukatili kwa watu wenye ualbino.
0 Comments