Kwa ufupi
Tatizo la ukosefu wa ajira ni la Dunia nzima. Wanavyuo wengi wameendelea kuzunguka huku na kule kuomba kazi bila mafanikio.
Kwa mujibu wa andiko la Umoja wa Mataifa, asilimia 20 ya vijana duniani kote hupata tatizo linalohusiana na afya ya akili kila mwaka. Kwa bahati mbaya hali hiyo hutokea katika kipindi cha kuhama kutoka utoto kuingia utu uzima, huku hali hiyo ikihusishwa na ukosefu wa ajira pamoja na sababu nyingine kama hizo. Andiko hilo lilitolewa mwaka jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili duniani ambayo huadhimishwa Oktoba 20 kila mwaka.
Tatizo la ukosefu wa ajira ni la Dunia nzima. Wanavyuo wengi wameendelea kuzunguka huku na kule kuomba kazi bila mafanikio. Wengi wamekaa zaidi ya miaka mitatu nyumbani tangu wamalize masomo bila kupata ajira.
Kama hiyo haitoshi waliobahatika kupata kazi nao wanaingia katika hali ya kutofurahia kutokana na kulipwa ujira mdogo usiokidhi mahitaji yao.
Takwimu zinaonesha kuwa kwa wastani soko la ajira nchini lina uwezo wa kuzalisha ajira zipatazo 300,000 kwa mwaka katika sekta rasmi ukilinganisha na wastani wa wahitimu 600,000 hadi 800,000 wanaoingia katika soko la ajira nchini.
Chanyamoto hii imekuwapo kwa muda mrefu kwa maana hiyo anayepaswa kukabiliana na tatizo hili la ajira ni kijana mwenyewe, kwa kuhakikisha anajipanga kwa ajili ya kujiajiri siku za usoni tangu akiwa masomoni.
Wakati umefika wa vijana kuachana na mawazo mgando kuwa ukiwa msomi lazima ufanye kazi ofisini kwenye kiti cha kuzunguka badala yake maamuzi yafanyike mapema kwa kuliondoa hilo kichwani.
Kwa kufanya hivyo kijana anapaswa kujiandaa kujiajiri kwa kutumia taaluma yake.
Taaluma ina uwezo wa kumsaidia kijana kuajiriwa au kujiajiri, kutokana na elimu aliyoipata na maamuzi sahihi aliyofanya wakati akichagua anasomea nini katika hatua ya elimu ya juu au ya awali.
Kijana wakati huu unaweza kuangalia namna gani unaweza kujiajiri kulingana na ulivyojipanga ukiwa shuleni, chuoni, lakini cha msingi zaidi ni kujitambua na kutambua elimu uliyoipata itakusaidia vipi na unaithamini kiasi gani.
Mambo yanayoweza kukusaidia kujiajiri ambayo pengine hata chuoni au shuleni hukufundishwa, ni kujumuika katika vikundi bila kujali upo na watu wa aina gani, lakini muhimu wake wenye mawazo chanya na mwamko wa mabadiliko.
Katika hili hakikisha wana mawazo kama yako. Isijiunge na watu wenye mawazo tofauti kwa sababu hamtafikia muafaka na kuchelewa kukifanya kile mlichokikusudia.
Jambo jingine unaloweza kufanya katika harakati za kujiajiri ni kutumia mazingira yaliyokuzunguka kutafuta fursa. Hapa unaweza kuangalia changamoto mbalimbali badala ya kuwa miongoni mwa walalamikaji, kwa kutumia weledi ulioupata masomoni, hiyo ikawa kwako ni fursa kwa kuitafutia ufumbuzi utakaokuingizia kipato.
Usiridhike na wazo moja kila mara tafuta mawazo mengine. La kwanza linapofanikiwa kwa sababu ajira hakuna wengi wataiga uliyoyaanzisha, hivyo kwa kuja na wazo jipya utakuwa unaongoza na kusonga mbele.
Pia, unaweza kutumia taaluma uliyonayo kama fursa ya kujiajiri kulingana na kile ulichokisomea kwa kuwa na mtandao mpana.
Hivyo ni vyema unapokuwa chuoni au shuleni kujiweka karibu na wale waliosoma taaluma kama yako hususani waliojiajiri au kuajiriwa sekta binafsi kwa sababu wao ni wabunifu zaidi.
Hii itakusaidia kujifunza mapema wao walifanya nini na wewe kunufaika na taaluma yako. Kumbuka kujiunga na taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na taaluma uliyosomea ili kupata ujuzi zaidi na kukutana na watu wengi watakaokupa “michongo” kama wasemavyo vijana wa mjini.
0 Comments