TUIJENGEE UWEZO KISWAHILI KUWA LUGHA YAKUFUNDISHIA

Kwa ufupi

Ni mdahalo uliokusanyisha wataalamu mbalimbali na ulijadili kwa kina mambo mengi, ingawa katika hitimisho kulikuwa na mapungufu kutokana na muda.Upande mmoja uliokuwa unaunga au kupinga mada hiyo haukupata nafasi nzuri ya kuhitimisha hoja kutokana na muda na hivyo ilikuwa vigumu kuchambua hitimisho la kila upande na kupata mwelekeo wa nini kinatakiwa kifuate.

Jumapili ya Machi 19, Chama cha Waandishi wa Kiswahili kwa kushirikiana na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) waliandaa kongamano kwenye Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kujadili Uamuzi wa Kutumia Kiswahili Katika Nyanja Mbalimbali.

Ni mdahalo uliokusanyisha wataalamu mbalimbali na ulijadili kwa kina mambo mengi, ingawa katika hitimisho kulikuwa na mapungufu kutokana na muda.

Upande mmoja uliokuwa unaunga au kupinga mada hiyo haukupata nafasi nzuri ya kuhitimisha hoja kutokana na muda na hivyo ilikuwa vigumu kuchambua hitimisho la kila upande na kupata mwelekeo wa nini kinatakiwa kifuate.

Nilifuatilia kongamano hilo kwa makini na wakati fulani niliona lilikuwa linapoteza mwelekeo na kujikita zaidi katika kutumia Kiswahili kufundishia hivyo wachangiaji kutumia matokeo ya tafiti nyingi zinazoonyesha kutumia lugha ya kwanza kufundishia huwezesha wanafunzi kuelewa vizuri.

Kwa maana nyingine, kongamano hilo lilikuwa limejikita katika kuangalia jinsi mfumo wa elimu ulivyoshindwa kutoa walimu wazuri wa lugha ya Kiingereza kuwezesha wanafunzi kuelewa masomo vizuri. Wale waliokuwa wanaunga mkono suala la kutumia Kiswahili kufundishia, hawakuweza kutuambia mazingira ya kuanza kutumia lugha hiyo yameandaliwa vipi kiasi cha kushawisha wengine kuwa muda umefika.

Mchangiaji mmoja kutoka Zanzibar alihoji kama visiwa hivyo vinazungumza Kiswahili tofauti na cha Bara, inawezekanaje lugha hiyo ikaanza kutumika wakati ni vitu viwili tofauti Bara na Visiwani.

Mchangiaji mwingine, Profesa Adolph Mkenda, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, aliunga mkono kutumia Kiswahili lakini akasema kunatakiwa kufanya uwekezaji ili suala hilo lifanikiwe. Alitoa mfano wa jinsi maneno mawili ya Kiingereza yalivyo na maana moja katika Kiswahili. Alisema neno “justice” na “right”, yote yana maana ya “haki” katika Kiswahili, lakini kwa Kiingereza ni dhana mbili tofauti.

Kulikuwa na changamoto nyingi zilizoibuliwa ambazo, kwa mtazamo wangu, wale wanaotaka Kiswahili kianze kutumika kufundishia walishindwa kuzitolea majibu ambayo yangeshawishi upande wa pili uone kuwa ni muda muafaka kuanza kukitumia kufundishia.

Nikiwa mdau wa Kiswahili, naona kuna mambo yanatakiwa kufanywa kabla ya kuanza kukitumia Kiswahili.

Ninayoyaona makuu ni mawili; kulazimisha Kiswahili kifundishwe kwa wanafunzi wa nyanja wa vyuo vya elimu ya juu, na kusanifu Kiswahili ili kiwe na sura moja kote nchini.

Ni ajabu tunataka kutumia Kiswahili kufundishia wakati huu ambao vijana wetu hawajivunii na wala hawaoni aibu kukosea kutamka au kutumia maneno ya Kiswahili. Na ukienda katika istilahi, wengi hawawezi.

Moja ya changamoto zilizoibuliwa na wengi waliopinga hoja ya kuanza kutumia Kiswahili, ni ukosefu wa istilahi za kutosha za kiisimu hasa katika masomo mfano ya sayansi na sheria.

Hili haliwezi kuja kwa siku moja au kwa kutunga maneno ambayo hata kuyatumia yanaleta ukakasi, kama Dk Michael Kadege alivyosema. Inahitaji utafiti wa hali ya juu.

Nachopendekeza, wahusika waandae mitalaa ya somo la Kiswahili kwa wanafunzi wa nyanja tofauti kwa vyuo vya elimu ya juu. Yaani wanaosomea uhandisi, basi waandaliwe mtalaa ambao utawafanya wajue istilahi nyingi za kiisimu katika taaluma yao.

Vivyo hivyo kwa wanafunzi wa sheria, sayansi ya siasa, sosholojia, udaktari na fani nyingine.

Somo hili likiwa la lazima kwa wanafunzi wote wa elimu ya juu, litajenga msingi kwa wahitimu wa fani tofauti kuwa na ufahamu wa istilahi za fani yao na kuzizoea kabla ya kuanza kuzitumia.

Baada ya miaka kama kumi hivi, Kiswahili hakitakuwa cha ajabu tena, hasa katika masomo kama hayo ya uhandisi, sheria, kemia, bailojia na mengine. Vyuo hivyo ndivyo vinavyotoa walimu kwa ajili ya shule za sekondari.

Baada ya hapo ukiwaambia watu kwamba tumeshafanya juhudi hizi na sasa Kiswahili kinaweza kuanza kutumika, wengi watakuelewa.

Naelewa kuwa juhudi kubwa zinafanyika kusanifu Kiswahili lakini hazionekani katika matumizi. Soma taarifa mbalimbali za Serikali, hotuba za bajeti za wizara hata wanasiasa wanapozungumza, utaona wengi hawatumii Kiswahili sanifu.

Na hoja kwamba Zanzibar wanatumia Kiswahili tofauti na cha Bara katika masomo, nalo linafaa lifanyiwe kazi. Kama mtihani ni mmoja na ndani ya nchi moja kuna lugha mbili za Kiswahili, ni wazi kuwa lengo la kutumia Kiswahili kufundishia halitafanikiwa.

Wote tuna hamu sana ya kuona Kiswahili kikianza kutumika kufundishia lakini hatuoni mazingira yanayojengwa kuwezesha hilo kufanikiwa. Hivyo, Tataki, Chama cha Waandishi wa Kiswahili na taasisi nyingine zilizojikita katika kuendeleza lugha hii, hazina budi kuhakikisha zinaweka mazingira yatakayofanikisha lugha yetu itumike kufundishia.

0 Comments