Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewataka wasomi na watafiti kuishauri serikali ni namna gani inaweza kuimarisha taasisi zake ili ziweze kusukuma azma ya nchi katika kujenga uchumi wa viwanda.
Akifungua Mkutano wa Mwaka wa Utafiti ulioandaliwa na Taasisi Inayofanya Utafifi wa Sera na Maendeleo ya REPOA, Dk Mpango alisema watafiti hao kutoka sehemu mbalimbali duniani, wahakikishe wanatoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sheria, sera na taratibu mbalimbali zinazohusika katika kujenga uchumi wa nchi.
Alisema kiuchumi unapozungumzia kuimarisha taasisi hayo ni masuala yanayohusu sheria, taratibu, sera, kanuni ambazo ndizo zinazotoa mwongozo katika kujenga uchumi wa nchi.
Alisema wasomi hao pia washauri namna gani taasisi kama Bunge, Mahakama, Jeshi na benki yanaweza kusaidia katika kujenga uchumi wa viwanda.
“Sisi tunaamini kuwa kama taasisi ziko legelege na hazikukaa vizuri, hili linaweza kupunguza kasi yetu ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda, ndio maana ninawauliza ninyi wasomi kwamba ni namna gani sasa tunaweza kuboresha hizi taasisi zetu?” alisema Dk Mpango.
Aliongeza kuwa, serikali kwa upande wake imechukua hatua kadhaa katika kuimarisha taasisi hizo, ikiwa ni pamoja na kupambana na vita dhidi ya rushwa.
Alisema wanachukua hatua hiyo kwa kutambua kuwa bila kumaliza rushwa, uchumi wa viwanda hauwezi kufanikiwa. Pia alisema serikali inataka kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya kiserikali kwa kuondoa urasimu katika taasisi zake.
Alisema lengo ni kutaka mwekezaji anapotaka vibali vya uwekezaji apate kibali hicho haraka iwezekanavyo.
Aliuambia mkutano huo unaohusisha washiriki takribani 300 kutoka sehemu mbalimbali duniani, kuwa serikali pia imeboresha mifumo yake ya kodi.
Alisema serikali inataka kushiriki katika biashara makini ambayo inafanywa kwa kuzingatia maadili ndani ya serikali na kwenye sekta binafsi.
Alisema dhamira ya serikali katika kujenga uchumi wa viwanda ni ya dhati na ndiyo maana inajielekeza zaidi katika kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu.
Alitoa mfano wa ujenzi wa reli, upanuzi wa bandari, ununuzi wa ndege mpya, miundombinu ya umeme na gesi, unadhihirisha kwamba malengo ambayo serikali imeahidi yanafikiwa.
Alisema pamoja na hatua zote hizo, serikali inatambua kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa ujuzi linalowakabili wananchi wake.
Alisema ndio maana kwa sasa wamejielekeza kuhakikisha kuwa wanatoa nafasi nyingi za mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana ili waweze kukabiliana na wimbi la ukosefu wa ajira nchini.
Mgeni maalumu kwenye mkutano huo, Profesa Lant Pritchett kutoka Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, alisema nchi yoyote ikitaka kuendelea ni kuhakikisha kuwa inafanyia kazi sera inazoziweka.
Alisema kuwa na sera peke yake haitoshi, bali kinachotakiwa ni namna ya kutekeleza sera hizo na matokeo yake kuonekana.
Aliishauri serikali kuhakikisha inakuwa na vipaumbele ambavyo inakwenda navyo badala ya kupeleka mambo mengi kwa wakati mmoja.
Alisema nchi inafanikiwa pale inapofanikiwa kutekeleza malengo iliyojiwekea.
“Tambueni tatizo, lishughulikie hilo. Mkimaliza nendeni katika jambo lingine,” alisema mtaalamu huyo aliyesisitiza kukabili rushwa, akisema ni adui namba moja katika uwekezaji.
0 Comments