Hivi karibuni, nilikuwa nimekaa mahala na bwana mmoja akanisimulia kisa cha mwanae anayesema ilikuwa bahati akaingilia kati mapema, vingine angeliharibika.
Anasema mwanae alikuwa ameanza kuwa na rafiki mtukutu, aliyeanza kumshauri kutega shule. Anasema ilifikia wakati mwanae anaaga kwamba anakwenda shule kumbe anaishia vichochoroni, sokoni na kuzurura huku na kule na wakati mwingine aliwahi kukamatwa na mwenziye wakiwa wameiba machungwa sokoni!
Anasema alipofuatilia ndipo waalimu wakamwaambia kwamba mwanae ni kijana mzuri lakini ameanza kupotoshwa na rafiki aliyempata siku za karibuni.
Waalimu wakamhakikishia kwamba rafiki huyo mpya wa mwanae hana malezi mazuri anakotoka, wazazi wake hawajali na hata wakiitwa shuleni hawaji na kwamba licha ya wa waalimu kuanza juhudi za kuwatenganisha, wakamtaka mzazi huyo asaidie katika hilo.
Yule mzazi mwenzangu akasema ni muhimu sana kwa mzazi kila unapopata nafasi kufuatilia mwanae njiani, kila anapokwenda na kutoka shule. Iwe anakwenda kwa miguu ama hata kutumia daladala na mabasi ya shule na lingine ni kujua marafiki zake na kufika hata nyumbani kwao.
Mzazi mwenzangu usijiridhishe tu kwamba mwanao anasoma shule ambayo ni jirani na nyumbani kwani inawezekana hapo njiani, kuna sehemu anapitia na siyo pazuri na pengine kuna mambo anafanya ama kujifunza ambayo unaweza kuyagundua ukifanya mazoea ya kumfuatilia nyuma na siku zingine kuvizia nyakati za kutoka shule.
Kwanza mtoto akigundua kuna siku unamfuatilia lazima atakuwa makini pia. Tukumbuke kwamba watoto ni wepesi pia kuiga ama kujifunza mambo ya hovyo na wengine ni waoga kusema mambo ya hovyo wanayokutana nayo hata kama hawayapendi na hasa pale mzazi unapokuwa hujengi ‘urafiki’ na mtoto.
Tuje sasa kwa watoto wanaosoma katika shule ambazo zina usafiri maalum, hususan hizi za binafsi. Ni kweli wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule hizi mijini ambazo zina usafiri maalum wa kuchukua watoto majumbani ama vituoni na kuwarudisha, wengi hawachukui dhima ya kufuatilia kinachotendeka hapo katikati kwa macho yao ama hata kwa kuuliza watoto kila siku wawaeleze kilichotokea njiani siku hiyo.
Wanachofanya wazazi wengi ni kumpeleka mtoto kituoni, kisha gari likija anampandisha kwenye gari na kusubiri atakapoletwa baada ya saa za shule, basi. Lakini zipo tuhuma kwamba kwenye mabasi haya kuna makondakta, ambao baadhi yao hawatofautiani sana na hawa walioko kwenye madaladala kitabia.
Yaani wanaweza kuwa na lugha za matusi na ukatili na hivyo kuwa chanzo cha kuwafundisha watoto wadogo tabia zisizofaa na hatarishi. Lingine muhimu kwa mzazi ni kujua ukarimu wa hao makondakta kwa watoto.
Je, watoto wanaposhikwa na mahitaji maalumu njiani, kama vile kutaka kujisaidia ama wale wa kike kutokewa na mahitaji maalum ya kike, wana uvumulivu wa kuchukua hatua kuwasaidia kabla ya kufika nyumbani?
Kwa vile magari haya yanabeba watoto wa kike na wa kiume huku makondakta wao, mara nyingi wakiwa vijana wadogo kati ya miaka 18 na 30 wa kiume swali linakuja; Je, tunawaamini vipi katika usalama wa hawa mabinti wadogo?
Ndio maana ninasema mzazi akiwa anafuatilia, kwa yeye mwenyewe hata kupanda gari hilo siku moja, kumuuliza maswali mwanae na hata mtoto mwingine wa jirani bila kusahau kumuona kondakta mwenyewe na dereva namna walivyo kwa macho, anaweza kujua mambo fulani na kuchukua hatua stahili.
Kinachofahamika ni kwamba baadhi ya magari haya yanamilikuwa na shule husika na mengine ni ya watu binafsi waliokubaliana na mashule hayo kutoa huduma hii.
Lakini ipo haja, wakati mwingine mwalimu fulani kuwemo kwenye ruti, hususan waalimu wa kike, ili kudhibiti miendendo mibaya inayoweza kuwa inatokea kwa kujirudia rudia kwenye magari haya na watoto wakanasa.
Watoto wanaokwenda shule kwa kutumia daladala ndio wanaoumiza kichwa zaidi. Lakini ninashauri sana kama mtoto anaweza kusoma shule ya karibu, mzazi jitahidi na iwe hivyo.
0 Comments