MKUU wa mkoa wa Ruvuma Dk Binilith Mahenge, amewata wazee katika mkoa huo kutumia muda wao kuwaeleza vijana umuhimu wa kutunza amani iliyopo kwa maendeleo.
Mkuu wa mkoa amesema hayo, wakati akizungumza na baadhi ya wazee kutoka katika maeneo mbalimbali ya manispaa ya Songea Ikulu ndogo mjini Songea.
Alisema kwamba maendeleo yatapatikana iwapo kutakuwa na amani sambamba na kuongeza juhudi za kazi.
Aidha Dk Mahenge,amewashauri vijana wanao jishughulisha na kazi ya kuendesha boda boda kuacha kufanya kazi hizo hadi usiku wa manane, kwani imebainika ni chanzo cha kuongezeka kwa matukio ya uhalifu.
Alisema, hata hivyo serikali kwa kutumia jeshi la polisi na vyombo vya dola itahakikisha inaimarisha doria katika maeneo yanayotumiwa na wahalifu hao, kwani wana sababisha raia wema kukosa uhuru na wasisafiri kwa amani.
Aidha Dk Mahenge akizungumzia mgao wa pembejeo za kilimo kwa msimu wa mwaka 2016/2017 alisema, mkoa ulipangiwa kupatiwa kiasi cha tani 2,456 za mbolea ya kupandia,tani 2,456 za mbolea ya kukuzia na tani 491 za mbegu bora ya mahindi kupitia utaratibu wa ruzuku,hata hivyo kiasi kilicholetwa kilikuwa kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya wakulima wa mkoa huo.
Mahitaji halisi ya pembejeo ni takribani tani 60,467.60 za mbolea ya kupandia na kukuzia ikiwemo mbegu za mahindi.
0 Comments