Kwa ufupi
Katika makala hii tutataja baadhi ya mambo ambayo mtu akiyazingatia ataweza kupata mafanikio makubwa katika maisha. Hususan, kumuwezesha kupata vitu adhimu anavyovihitaji katika uhai wake. Mambo hayo ni haya yafuatayo:-
Wakati fulani niliwahi kuwauliza ndugu na jamaa ninaowafahamu wanitajie vitu wanachohitaji ili waone kuwa wamefanikiwa katika maisha. Walitaja vitu vingi lakini vilivyotajwa sana vilikuwa kazi nzuri ya kuajiriwa au ya kujitegemea, nyumba nzuri, familia bora, gari ya kisasa shamba, kipato cha kutosha kwa mahitaji muhimu ya maisha na hadhi katika jamii. Lakini kila niliyemuuliza kama amefanikiwa kuvipata vitu hivyo alikataa na kusema amefanikiwa kupata vichache tu. Nilipowauliz.a wanakusudia kufanya nini ili wapate vitu ambavyo hawajavipata. Wengi walionyesha mashaka
Katika makala hii tutataja baadhi ya mambo ambayo mtu akiyazingatia ataweza kupata mafanikio makubwa katika maisha. Hususan, kumuwezesha kupata vitu adhimu anavyovihitaji katika uhai wake. Mambo hayo ni haya yafuatayo:-
Kutambua dhamira
Kama ilivyo kwa mtu anayetarajia kwenda safari hawezi kukurupuka tu na kwenda bila kujua anakwenda wapi, kwa lengo gani na kujua atakavyofika aendako. Kanuni ya kwanza kwa jambo lolote unalotarajia kufanya na kupata mafanikio ni kujibainishia wewe mwenyewe katika nafsi, dhamira yako na kuweka mkakati wa jinsi utakavyofanikisha lengo lako. Hakuna jambo lolote katika maisha ambalo unaweza kulifanikisha bila kuweka mpango wa utekelezaji ambao licha ya kuweka malengo na mkakati, utadhihirisha vitu vingine kama nyenzo zitakazohitajika muda wa utekelezaji na viashirio vya mafanikio.
Ujuzi na ustadi
Ujuzi ni jambo jingine muhimu kwa kupata mafanikio katika jambo lolote unaloweza kuamua kufanya. Kuna baadhi ya mambo ambayo hata tukifanya juhudi na kuwa makini hatuwezi kuyafanikisha bila kuwa na ujuzi. Wakati tunapoyakinisha dhamira na kuweka malengo na mikakati hatuna budi kufikiria kama tuna ujuzi wa kitu tunachotaka kufanya. Kama hatuna, inabidi tujiulize jinsi tunavyoweza kuupata. Iwapo hatutakuwa na hakika ya kuupata, tutalazimika kufikiria kufanya shughuli nyingine.
Ujasiri
Wanasaikolojia hutuasa kuwa ujasiri una umuhimu wa pekee katika jambo lolote tunaloamua kufanya katika maisha. Tulio wengi huwa hatufanikiwi kutokana woga. Tunatawaliwa na kauli kama vile “Kweli mimi nitaweza?” Swali hili huwa tunaliwaza katika mawazo yetu hadi tukaogopa kujaribu kufanya kila kitu.
Woga hutufanya wakati mwingine tushindwe hata kufanya mambo ambayo tungeweza kuyafanya bila wasiwasi wowote. Siri ya mafanikio katika maisha ni kuwa na ujasiri wa kuthubutu kufanya hata kama matokeo yake yanaweza kuwa na mashaka ya kuwa sahihi.
Mawasiliano sahihi
Imethibitisha kuwa mawasiliano hafifu huathiri kwa kiwango kikubwa ushirikiano na maelewano baina ya watu katika shughuli mbalimbali kama vile ujasiriamali, elimu, utamaduni na hata mahusiano ya mtu binafsi na jamii. Maelewano mabaya na hali ya kutoelewana husababishwa na mawasiliano hafifu. Hivyo, kuwa na uwezo wa kuridhisha wa lugha na mbinu za mawasiliano ni fursa muhimu katika mafanikio ya aina yoyote katika maisha.
Ucheshi
Ucheshi ambao huambatana na uchangamfu ni nyenzo muhimu sana katika shughuli za aina zote ambazo tunalazimika kukukatana watu. Kwa hakika hakuna mafankio yoyote ambayo mtu anaweza kuyapata bila kupitia kwa watu wengine. Kinachoweza kuwafanya watu wawe karibu nawe, wakavutiwa na wewe na kuhisi kuwa wanakuhitaji ni ucheshi wako.
Ucheshi ni dalili ya upendo na wala huwa hauna gharama yoyote, kwani hata tabasamu inatosha sana. Jambo muhimu ni kuepuka kabisa ucheshi wa kinafiki maana hauwezi kumfikisha mtu kwenye mafanikio yeyote yanayotokana na watu. Tena huweza kusababisha chuki.
Kujiamini
Kama isivyofaa kwa mtu kuwa na woga, kutojiamini ni hulka inayokwamisha mafanikio. Kujiamini hutokana na mambo mawili makuu ambayo ni kuwa na ujuzi na kile unachofanya na hali ya kujitambua wewe mwenyewe. Ingawa baadhi ya watu huzaliwa na kipaji cha kujiamini na kujitambua, lakini kila mtu akijituma na kudhamiria kwa dhati anaweza kuiibua na kuijenga hulka hii ambayo kila mtu huwa nayo. Tunapoongeza uwezo wa kujiamini ndipo tunapoimarisha uwezo wa kutenda. Na kadri ustadi wa kutenda unavyoimarika ndivyo kadri hali ya kujiamini inavyoongezeka.
Msimamo
Kuna baadhi ya watu ambao wanapokuwa wakishughulikia jambo fulani huona ni rahisi tu kuamua kuliacha jambo hilo wanapogundua mkwamo au kikwazo cha aina yeyote, hata kama ni kidogo tu. Huu ni udhaifu ambao kila mtu mwenye lengo la kupata mafanikio katika maisha anapaswa kuuepuka. Kama unaamini katika lengo ulilojiwekea na una hakika na matarajio uliyoyakusudia kuyafanikisha ni lazima uwe imara katika msimamo. Kamwe usiwe na hisia katika nafsi yako kuwa ukishindwa utaweza kuacha. Kwani hisia hizo zitatawala akili yako na kukufanya ujihisi umeshindwa hata kama usingeshindwa. Hata kama itabidi ubadili hisia zako katika namna ya utekelezaji fanya hivyo lakini usiache kujituma kukamilisha jambo aliloliwekea lengo.
Ridhika na hatua unazofikia katika utekelezaji.
Unapokuwa katika harakati za utekelezaji wa jambo uliloamua kufanya huwa budi kuifurahia kila hatua ya mafanikio utakayokua umeifikia. Kwa kufanya hivyo utapata hamasa itakayokuongezea matumaini na kukataa kukata tamaa au kukubali kushindwa.
0 Comments