Kwa ufupi
Miongoni mwa vijana hapa nchini wanaoendana na usemi huo ni pamoja na Kennedy Mpumilwa ambaye ni mmiliki na mkurugenzi wa shule ya Msingi Kellys, iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Bidii, kujituma na kutokata tamaa ni miongoni mwa siri zinazotajwa katika maisha mwanadamu yoyote na kuwa hakuna njia ya mkato katika maisha.
Miongoni mwa vijana hapa nchini wanaoendana na usemi huo ni pamoja na Kennedy Mpumilwa ambaye ni mmiliki na mkurugenzi wa shule ya Msingi Kellys, iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Mpumilwa anasema baada ya kumaliza elimu yake ngazi ya stashahada ya elimu alihangaika kutafuta kazi lakini baada ya kuzunguka kila kona na kukosa kazi alipata wazo la kuanzisha kampuni yake ya Kedas Business & Building Agent inayoshughulika na masuala ya ardhi ili aweze kufungua shule kwa baadaye.
“Niliona nifungue kampuni ili niweze kupata kuanzisha shule na nilianza na wanafunzi wanne na sasa nina wanafunzi 200,” anajinasibu.
Anafafanua kwamba kwa sasa ana wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tano na kati ya hao wapo 32 ambao wanaishi katika mazingira magumu.
Haikuwa safari rahisi Mpumilwa anasema alianza kufundishia nyumbani kwake, lakini baadaye alipata eneo na kuanza kuwafundishia chini ya mti lakini kwa sasa amefanikiwa kuwa na madarasa tisa ya wanafunzi.
“Mimi taaluma yangu ni mwalimu na nilipenda siku moja nimiliki shule yangu ila tatizo lilikuwa ni mtaji. Nilipambana huku na kule kutafuta fedha kwa wafadhili mbalimbali na waliisaidia baada ya kuona juhudi zangu,” anasema Mpumilwa.
Anasimulia akiwafundisha wanafunzi chini ya mti baadhi ya watu wakiwemo marafiki zake walimcheka na hata baadhi yao walimtolea maneno kwamba ameanza kuwehuka na kufilisika kiakili.
Anasema kwamba wakati anatafuta wafadhili alienda katika benki ya Meru Community iliyopo Leganga mkoani hapo na kufanikiwa kupata mkopo wa Sh9 milioni ambapo alichukua Sh7 milioni na kujenga darasa moja na fedha nyingine alinunulia samani na kufanya usajili wa shule yake.
Malengo yake ni kuhakikisha wanafunzi wake wanafikia elimu ya chuo kikuu kwa kuwa anaamini ukitaka kuikomboa jamii ni lazima kwanza watoto wapate elimu.
Hata hivyo anatoa ushauri ya kwa vijana nchini kuachana na dhana ya kusoma ili wapate kuajiriwa bali wanapaswa kutafuta mbinu za kujiajiri na kusisitiza waachane na uvivu na woga.
Anafafanua kwamba laiti kama akipata nafasi ya kukutana na Rais John Magufuli angemshauri kuanzishwa kwa vyuo vya ufundi katika kila kata ili vijana wapate nafasi ya kujifunza mbinu za ufundi.
0 Comments