Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
UKITAFAKARI kwa kina kuhusu kupotea kwa maadili ya taifa utagundua kuwa hata huu mfumo wetu wa elimu unachangia. Elimu nchini na Afrika kote ilianza kama chombo cha kuandaa vijana wake kuchukua nafasi yao katika jamii ya Afrika.
Uzoefu wa elimu ya Kiafrika ilianzishwa hasa kuandaa vijana kwa jamii katika jumuiya ya Kiafrika na siyo kwa maisha nje ya Afrika. Elimu katika jamii yetu ilijumuisha mambo kama sanaa, sherehe, michezo, matamasha, dansi, kuimba, na kuchora. Wavulana na wasichana walifunzwa wakiwa wametenganishwa kusaidia kuandaa kila kikundi kwa majukumu yao kama watu wazima.
Wakati ukoloni na ubeberu wa Ulaya ulipoingia ulianza kubadili mfumo wa elimu wa Kiafrika. Shule ikawa haihusu tena mila, shule sasa ikamaanisha kupata elimu ambayo ingeweza kuwaruhusu Waafrika kushindana na nchi kama vile Marekani na zile zilizoko Ulaya. Afrika ikaanza kuzalisha wanafunzi wao wenyewe walioelimishwa kama vile wa nchi zingine.
Hata hivyo, viwango vya ushiriki katika nchi nyingi za Afrika ni vya chini. Mara nyingi shule zetu hukosa vifaa vingi vya msingi, na vyuo vikuu vya Afrika vinakabiliwa na msongamano na wakufunzi wanaovutiwa kwenda nchi za Magharibi kwa malipo na mazingira bora zaidi. Lakini baadhi ya nchi za Kiafrika wamejitahidi kuboresha mifumo ya elimu yao iendane na mazingira yao, ndiyo maana zimepiga hatua kubwa katika maendeleo.
Hapa Tanzania, ukiangalia matatizo mengi yanayochangia kuporomoka kwa uchumi wa Tanzania utagundua kuwa yamejikita zaidi katika mfumo wetu wa elimu. Na ukichunguza kwa makini zaidi utaona kuwa matatizo yetu yapo kwenye kila ngazi ya jamii: kuanzia Taifa hadi kitongoji na ufisadi ambao sasa serikali ya awamu ya tano inapamba nao ulikuwa umeshika mizizi kila idara ya jamii, si serikalini tu bali hadi kwenye vyama vya siasa, na kwenye sekta binafsi.
Kuna changamoto nyingi zinazoukabili mfumo wetu wa elimu, mintarafu suala zima la kutoa wanafunzi watakaokuwa na maadili mema, wanafunzi wanaochukia rushwa, wananchi walio tayari kuwajibika kwa taifa lao na siyo vinginevyo. Pia kuwapo kwa taasisi nyingi zinazosimamia na kudhibiti kitu kimoja kunachangia kuwepo migogoro ya kiutendaji baina ya taasisi husika na hivyo kusababisha kudorora kwa elimu.
Kwa mfano; Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limeachwa kufanya tathmini ya elimu ya msingi, sekondari na elimu ya mafunzo ya ualimu huku Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (Veta) ikisimamia usajili na udhibiti wa taasisi zote za mafunzo ya ufundi stadi nchini. Pia kuna taasisi zingine zinasimamia elimu ya juu: Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), linadhibiti taasisi za elimu ya mafunzo ya ufundi na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), inadhibiti vyuo vikuu vyote nchini.
Hivi sasa elimu ya msingi si ya msingi tena kama ilivyokuwa miaka michache baada ya uhuru kwani msingi unapaswa uwe imara siku zote. Wakati tumeingia kwenye kutoa elimu bure, jambo ambalo ni zuri sana lakini ni lazima liende sambamba na kuifanya elimu ya msingi kuwa msingi kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya ambao wamefaulu sana katika kuimarisha elimu ya msingi.
Nchini mwetu, miaka ilivyokuwa inazidi kwenda ndivyo ubora wa elimu Tanzania ulivyokuwa unashuka; ukichunguza kati ya wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi kati ya miaka ya 1980, miaka ya 1990 na miaka ya 2000 utagundua kuwa wote hao wana uelewa tofauti tena mkubwa tu. Pia inashangaza kwa nini hakuna masomo maalumu kwa maeneo maalumu yanayoendana na mazingira yao.
Ni muhimu waandaaji mitaala yetu, hata kama bado elimu yetu ni moja (centralized), wawe wabunifu kwa kubuni mitaala inayoendana na mahitaji ya ulimwengu wa sasa badala ya kuifanya elimu yetu iendeshwe kisiasa. Je, tulipoamua kuelekea kwenye Tanzania ya Viwanda, tumebadilisha pia mwelekeo wetu wa mitaala kujielekeza huko? Tunaimarishaje na kuhamasisha usomaji wa masomo ya sayansi? Na je, tumeandaa waalimu wa kutosha?
Elimu yetu kuanzia shule ya msingi hadi Chuo Kikuu mfumo wake hauendani na matakwa husika, umekuwa ukiendeshwa kwa mtindo wa chukua notisi nenda kajisomee (kakariri) halafu yote uliojifunza mhula mzima njoo uyajibu ndani ya saa mbili na hizo saa mbili ndiyo mustakabali wako mzima! Jambo jingine katika mfumo wetu wa elimu; mwanafunzi wa Kitanzania anakabiliana na kikwazo kikubwa cha lugha katika mafunzo yake.
Kwenye mtihani, akiulizwa swali kwa Kiingereza itambidi alitafsiri kwanza kwa Kiswahili (wakati mwingine hulitafsiri tena kwa lugha ya kwao), kabla ya kutoa jibu ambalo bila shaka itabidi lifuate mtiririko huohuo kwa kuugeuza. Juzijuzi kulikuwa na mjadala wa lugha gani itumike kufundishia. Mimi ninadhani ni wakati mwafaka wa kupunguza lugha moja kati ya Kiswahili na Kiingereza ili kuleta ufanisi zaidi.
Sina ugomvi wa lugha ipi itumike, lakini serikali inapaswa kuwa na sera madhubuti ya lugha. Wakati umefika tukubaliane kutumia lugha moja ya kufundishia, na isiwe ni makubaliano ya kisiasa tu na kama tunaendelea na Kingereza ni sharti tuwe na waalimu wazuri watakaofundisha vyema watoto wetu lugha hiyo kuanzia elimu ya awali hadi sekondari kuliko ilivyo sasa.
Lakini hii haina maana kuwa tukitumia lugha moja tutakuwa hatutumii nyingine, kwani kwa mtazamo wangu Kiingereza bado ni muhimu sana kwenye mawasiliano ya kimataifa na kinachotakiwa ni kufundishwa vizuri kuanzia chekechea na hili lisiachiwe shule binafsi zinazofundisha kwa Kiingereza pekee, bali hata shule za serikali. Tukiamua, wataalamu wetu wakashauri vyema, ninaona Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli inaweza.
Hii sera ya sasa ya wanafunzi kuanza na Kiswahili wakiwa shule ya msingi, na kufundishwa kwa Kiingereza wanapoanza sekondari ni kuwadumaza kifikra. Matokeo yake wanafunzi wa Kitanzania wanajikuta wakiwa hawajui Kiswahili wala Kiingereza. Staili hii ya ufundishaji imekuwa ikizima vipaji vingi na kuvilazimisha kukariri na mwisho kuviandaa vipaji hivyo kuwa mafisadi, ufisadi unaoanzia kwenye wizi wa mitihani.
0 Comments