ZAIDI ya wanafunzi 150 katika Shule ya Sekondari New Kiomboi wilayani Iramba mkoani Singida hawana vyumba vya kusomea baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo kuezua mabati yaliyoezekwa kwenye madarasa hayo.
Kutokana na athari hiyo, wanafunzi hao wanalazimika kusomea kwenye majengo mawili ya vyumba vya maabara viliyopo shuleni hapo.
Mkuu wa shule hiyo, Lameck Ayeiko, alisema tukio hilo lilitokea wiki iliyopita ambapo mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha kwa muda wa nusu saa tu, lakini ikaleta uharibifu mkubwa ikiwemo pia Ofisi ya Mkuu wa shule na ofisi za walimu.
“Kadhalika, ofisi yangu pamoja na ofisi ya walimu ziliezuliwa paa na maji yakajaa ndani,” alieleza Ayieko na kuongeza kuwa, zaidi ya Sh milioni 20 zinahitajika kurudisha majengo hayo katika hali yake ya kawaida.
Kutokana na tukio hilo, alisema waliitisha mkutano wa hadhara na kukubaliana kuwa kila mzazi achangie Sh 10,000 tu kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Emmanuel Luhahula alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba baada ya kufanyika tathimini ya uharibifu huo walibaini kuwa zaidi ya Sh milioni 20 zinahitajika kurejesha majengo hayo katika hali yake ya kawaida.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Linno Mwageni alisema ingawa baadhi ya majengo ya shule hiyo yalijengwa chini ya Programu ya Kuboresha Ujenzi wa Shule za Sekondari (SEDP), majengo yaliyoezuliwa hayahusiki kwa vyovyote vile na programu hiyo kwa kuwa ni ya zamani.
0 Comments