SERIKALI ITAFAKARI UPYA KUWAHAMISHA WALIMU

Serikali itafakari upya kuwahamishia walimu wa sekondari kwenda shule za msingi.



Kwa ufupi

Uamuzi huo kwa mujibu wa vyombo vya habari, ulitangazwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Elimu, Benard Makali, mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).Sababu alizozitoa ni kwamba katika shule za sekondari za serikali, walimu wa sanaa ni wengi kiasi kuwa ziada ya walimu 7,463, hivyo hawana budi kupelekwa shule za msingi ambazo zina upungufu wa walimu 47,157.

Hivi karibuni Serikali ilitangaza mpango wa kuwahamishia walimu wa sekondari wa sanaa kwenda kufundisha shule za msingi.

Uamuzi huo kwa mujibu wa vyombo vya habari, ulitangazwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Elimu, Benard Makali, mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Sababu alizozitoa ni kwamba katika shule za sekondari za serikali, walimu wa sanaa ni wengi kiasi kuwa ziada ya walimu 7,463, hivyo hawana budi kupelekwa shule za msingi ambazo zina upungufu wa walimu 47,157.

Pia, alisema walimu hao wanapelekwa shule za msingi kuboresha daraja hilo la elimu na kuwa majaribio tayari yameanza mkoani Arusha kabla ya kuelekea mikoa mingine.

Pamoja na ukweli kuwa mpango huo umefanyiwa majaribio, kuna mashaka na aina ya majaribio yaliyofanyika kwa muda mfupi na Serikali ikajiridhisha kwamba unafaa bila kufikiria athari za muda mrefu.

Kwa mfano, kitaaluma mwalimu amekwenda chuo kusomea taaluma yake ya ualimu kwa ajili ya kufundisha sekondari, siyo elimu ya msingi.

Taaluma ya ualimu ni zaidi ya kiwango cha elimu cha mtu. Ualimu ni kuwa na njia na mbinu za kumfundisha mwanafunzi kulingana na umri na kiwango chake cha kielimu.

Ualimu ni kuelewa saikolojia ya mwanafunzi kulingana na umri wake. Ualimu ni kuwa na ujuzi wa kutoa ushauri na kunasihi kulingana na umri wa mwanafunzi.

Kwa hiyo, mwalimu wa kiwango cha sekondari, mafunzo yake yalijikita kumfundisha mwanafunzi wa sekondari na siyo wa msingi. Vinginevyo ni kukoroga mambo.

Pili, walimu wa sekondari hapa nchini walisomea ualimu pamoja na somo moja au masomo mawili ya kufundishia, tofauti na walimu wa msingi ambao wanasoma masomo yote yaliyopo katika mtalaa wa elimu ya msingi.

Ingawa mbinu na njia za kufundishia zinaweza kuwa zilezile, lakini kwa mwalimu aliyesomea kufundisha sekondari atapata wakati mgumu kufundisha shule za msingi.

Tatu, kuna athari za kisaikolojia. Mwalimu aliyekwenda chuo kwa ajili ya kufundisha sekondari, akafanyia majaribio yake ya kufundisha sekondari, akaajiriwa sekondari; mwalimu huyu unapompeleka shule ya msingi, unamtafutia matatizo ya kisaikolojia.

Atakwenda kwa sababu mwajiri anayemlipa mshahara amesema na siyo kwa sababu anapenda au ameamua. Ni uamuzi utakaokuwa wa manung’uniko moyoni na utakaomfanya kuwa na msongo wa mawazo utakaoshusha ari ya utendaji wake.

Hoja kwamba kuwapeleka walimu wa sekondari shule za msingi ni kuboresha elimu ya msingi ni mawazo yasiyo na utaalamu ndani yake.

Kuboresha elimu kunahitaji mipango, sera na utekelezaji madhubuti kwa kuweka mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia, miundombinu bora, walimu bora na wa kutosha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Ni vema Serikali ikawaacha huko huko sekondari walimu hao ili kuendelea kuziba nafasi za walimu wanaoendelea kupungua kutokana na kustaafu, kuacha kazi na hata kufariki dunia, kuliko kuwahamishia msingi na baada ya muda mfupi upungufu unarudi palepale. Aidha, walimu wanaohitajika shule za msingi ambao ni zaidi ya 40,000, kuwapeleka walimu wasiozidi 8,000, hakutatui tatizo.

Ikiwa ni lazima walimu wa sekondari wahamishiwe shule za msingi, itakuwa vema wakarudi chuoni kwa ajili ya kufundishwa njia na mbinu za kumfundisha mwanafunzi wa shule za msingi.

0 Comments