SIDO YATOA MBINU ZA KUJIAJIRI KWA VIJANA- MTWARA


Meneja wa SIDO Mkoa wa Mtwara, ndugu Joel Chidabwa akiwatunukia vyeti wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali na matumizi ya vipodozi kwa wanawake wa mkoa wa Mtwara. Ndg. Chidabwa alifunga rasmi mafunzo hayo ya wiki mbili yaliyoandaliwa na kutolewa bure na taasisi ya Manjano Foundation mkoani Mtwara.Katika mafunzo hayo ya ujarisiamali na matumizi sahihi ya vipodozi, yalitolewa kwa wanawake 30 walionufaika na mafunzo hayo kupitia vipodozi vya LuvTouch Manjano vilivyo dhaminiwa na kampuni ya Shear illusions.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na wataalamu wa mambo ya biashara wakishirikiana na maofisa wa taasisi ya Manjano. Lengo ya mafunzo hayo ni kumwezesha mwanamke wa Kitanzania kuweza kujiajiri na kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa kujikita katika tasnia ya urembo na vipodozi. Mafunzo hayo yameshafanyika kwenye mikoa saba nchini, nayo ni Dar es Salaam, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Zanzibar, Dodoma na Arusha. Mpango endelevu wa taasisi ya Manjano Foundation ni kufikia mikoa 30 nchini ndani ya miaka mitano.

Baada ya wanawake hawa kuhitimu mafunzo hayo, taasisi ya Manjano Foundation inawaunganisha na Taasisi za Fedha zinazotoa mikopo bila riba au yenye masharti nafuu ili waweze kupata mtaji wa kununua bidhaa za vipodozi kwa ajili ya kuwawezesha kuanzisha biashara wakiwa chini ya uangalizi maalum wa Taasisi hiyo kwa mwaka mzima. Lengo ni kuhakikisha kila mhitimu wa mafunzo haya anapiga hatua na kuweza kujitegemea na kusaidia familia yake.

Washiriki walionufaika kwenye Mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja na Meneja wa SIDO Mkoa wa Mtwara, ndugu Joel Chidabwa.

Wanawake wa mkoa wa Mtwara walionufaiki na mafunzo ya ujasiriamali na urembo wamemshukuru afisa mtendaji mkuu wa Shear illusions na muasisi wa Taasisi ya Manjano Foundation mama Shekha Nasser kwa moyo wake wa kujitolea na kuwajali wanawake wengine hususani wakazi wa Mtwara. Wakiongea zaidi wanawake hao ambao wamepatiwa elimu ya biashara kutambua nafasi yao katika jamii inayowazunguka pamoja na namna ya kupamba maharusi, ueledi na jinsi ya kupata masoko na kuongeza mauzo kwenye biashara na matumizi sahihi ya vipodozi. Wamemshukuru mama Shekha kwa moyo wenye kuwajali na kuwabeba wanawake wenzake na kutoa elimu ya bure aliyokuwa nayo kwa wengine ili waweze nao kujiongezea kipato na kupunguza ukali wa maisha. Wameahidi kuyatumia mafunzo hayo kwa lengo la kujikwamua na tatizo la ukosefu wa ajira kwa wanawake na pia kujiongezea kipato.

0 Comments