TUMEDHAMIRIA KUWAWEZESHA WAANDISHI WA VITABU- TMF


Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura

Kwa ufupi

Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura alisema hayo juzi kwenye uzinduzi wa kitabu cha ‘Nguvu yangu dhidi yao’ kilichoandikwa na mwandishi wa habari Gordon Kalulunga.

Mbeya. Katika kuwawezesha wanahabari waliojikita kwenye utunzi wa vitabu, Taasisi ya Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) imeandaa mkakati wa kuwaendeleza ili kuinua vipaji vyao.

Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura alisema hayo juzi kwenye uzinduzi wa kitabu cha ‘Nguvu yangu dhidi yao’ kilichoandikwa na mwandishi wa habari Gordon Kalulunga.

Maudhui ya kitabu hicho, ni usaliti, rushwa, kuwakumbusha wabunge wajibu wao, kueleza umuhimu wa kijana wa Afrika kulinda utamaduni wao.

Sungura alisema licha ya TMF kujikita zaidi kuwawezesha waandishi wanaondika habari na kuzichapisha kwenye vyombo vyao vya habari, lakini kuna haja ya kuwawezesha wanaotaka kuandika vitabu.

“Tumeandaa mpango wa kuwawezesha wanahabari wanaoonyesha kujenga hoja zao kwa maandishi ya kudumu, wanazozifanyia uchunguzi wa kutosha na mwisho wa siku wanaandika kitabu ambacho ni kumbukumbu,” alisema.

Akizungumzia hilo, Mwandishi Kalulunga alisema changamoto kubwa kwa waandishi wa vitabu ni uchapishaji na ukosefu wa fedha.

“Uandishi wa vitabu unahitaji mtaji, waandishi wengi tumekuwa tukisita kuandika kutokana ukosefu wa mtaji ambao utasaidia katika uchapishaji na kusambaza ili kuwafikia wasomaji,” alisema Kalulunga.

0 Comments