Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
SERIKALI imesema inaandaa wataalamu watakaojielimisha kuhusu masuala ya nishati ikiwemo mafuta na gesi ili kufikia malengo ya kuwa na umeme mwingi wa uhakika na bei nafuu utakaotumiwa na Watanzania wote.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Nishati kupitia Mradi wa Tanzania na Uholanzi wa Masuala ya Nishati (TDECB).
Profesa Muhongo alisema jukwaa hilo linalenga kutoa mchango katika sekta za nishati mbadala na gesi kupitia tafiti zenye viwango, wataalamu na kusaidia katika sera ya nchi kuhusu masuala hayo.
Alisema vyuo ambavyo vimelengwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Zanzibar pamoja na vyuo vitatu kutoka nchini Uholanzi.
Alisema vyuo hivyo vitawezeshwa kupata vitendea kazi, mafunzo kuhusu nishati na watasaidiwa katika masuala ya sera.
Alieleza kuwa barani Afrika watu wasiopata nishati ni asilimia 46, na kwa nchini, vijijini watu wenye fursa hiyo ya kupata nishati ni asilimia 49.5, Tanzania nzima inapata umeme kwa asilimia 67.5 huku katika miji yote ni asilimia 97.5 hiyo ni kutokana na takwimu za Desemba mwaka jana.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Udsm, Profesa Florens Lugano alisema malengo ya jukwaa hilo ni kufikisha Tanzania kukuza uchumi wa viwanda, kutengeneza nafasi za ajira na kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla.
Profesa Lugano alisema pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili sekta hiyo, sera zilizopo zimesaidia kuleta mafanikio makubwa yanayoonekana.
0 Comments