WENYE VYETI FEKI JIANDAENI KUNG'OKA

Wenye vyeti feki kukumbana na rungu la JPM punde tu

Rais John Magufuli akikagua baadhi ya vyumba wakati wa uzinduzi wa majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la Mlimani jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni makamu mkuu wa Chuo chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala. Picha Ikulu

Kwa Ufupi

Rais alisema hayo jana wakati akizindua majengo ya mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), yaliyojengwa na Wakala wa Majengo (TBA) ambayo yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema anasubiri kukamilika kwa ripoti ya uchunguzi ili afanye uamuzi wa sakata la vyeti feki.

Rais alisema hayo jana wakati akizindua majengo ya mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), yaliyojengwa na Wakala wa Majengo (TBA) ambayo yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840.

Sakata la vyeti vya kughushi limekuwa kubwa baada ya mmoja wa wateule wa Rais Magufuli, kutuhumiwa kuwa anatumia vyeti vya kughushi baada ya kufeli elimu ya sekondari na kusababisha watu mbalimbali kumsihi mkuu huyo wa nchi atengue uteuzi wake.

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wamezungumzia elimu ya mteule huyo kwenye vikao vya Bunge, wakitaka Rais atengue uteuzi wake, huku Meya wa Ubungo, Boniface Jacob akiliwasilisha suala hilo mbele ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Wakati Askofu Josephat Gwajima akisema kuwa ana ushahidi wa suala hilo, msanii Nay wa Mitego pia amefyatua wimbo wa “Wapo” unaosema mtu anayeitwa Daudi Bashite ndiye jipu jipya nchini na kuhoji sababu za Rais Magufuli kutotengua uteuzi wake.

Baada ya kimya cha muda mrefu, Rais Magufuli alisema katika hafla ya uzinduzi wa barabara za juu katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Sam Nujoma, kuwa wananchi wasipoteze muda kuzungumzia mambo ya mitandaoni na kumtaka mteule huyo kuendelea “kuchapa kazi”.

Lakini jana, Rais aligusia kwa kifupi suala la kughushi vyeti wakati akizindua mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani.

0 Comments