Dhana ya kuwekeza katika sekta ya michezo kwa vijana wadogo wa shule za Sekondari imekua ikileta manufaa makubwa kwa Taifa katika kuzalisha wachezaji mahiri ambao wamekua wakipeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje ya chini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe alipokua akifungua michezo ya COPA UMISSETA ambayo inashirikisha shule za Sekondari za Serikali na Binafsi leo katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
“Nimefurahishwa na juhudi zinazofanywa na Kampuni ya CocaCola katika kuhakikisha tunaimarisha sekta ya michezo kwa vijana wadogo wa sekondari kwani kwa kufanya hivyo tunaibua vipaji na kuviendeleza kwa kupata wanamichezo mahiri wa baadaye” amesema Waziri Mwakyembe.
Aidha aliongeza kuwa Serikali itahakikisha kuwa inawekeza katika michezo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kuwa michezo ni ajira inayowapatia vijana riziki pamoja na kuchangia katika uchumi wa nchi.
Vilevile aliwataka walimu kufuata ratiba za vipindi vya michezo kwa kuhamasisha michezo mashuleni ikiwemo kuwapatia wanafunzi nafasi ya kujifunza na sio kuvitumia vipindi hivyo kwa shughuli nyingine.
Hata hivyo Mhe. Mwakyembe aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanawapatia watoto wao nafasi ya kucheza na kujifunza michezo mbalimbali inayowajenga kimwili na kiakili.
“Michezo inafaida kubwa kwa afya ya binadamu ikiwemo kuimarisha akili na mwili, kujenga ushirikiano na urafiki baina ya watu “ alisema Mhe. Mwakyembe.
Naye Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Kampuni ya CocaCola Bw. Eric Ongara alisema kuwa Kampuni ya CocaCola inaamini katika kuibua vipaji kuanzia ngazi ya chini ndio maana wamekua wakidhamini mashindano hayo.
Pia aliongeza kuwa Kampuni ya Coca-Cola itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa michezo inazaa matunda na kufikia lengo lililokusudiwa la kuibua vipaji vya michezo na kuviendeleza.
Michezo ya COPA UMISSETA ilifunguliwa rasmi Mjini Dodoma Aprili 28 mwaka huu ambapo kitaifa yanatarajiwa kuanza Juni 6 hadi 15 mwaka huu katika Viwanja vya Chuo cha Ualimu Butimba Jijini Mwanza .
0 Comments