Kwa ufupi
Katika hatua zote ambazo nchi yetu imepita, wapo watu wenye umaarufu na wasiokuwa nao, ambao wako nyuma ya historia. Watu hawa ama walikuwa waasisi wa historia hiyo au waliwezesha tu iandikwe.
Tangu nchi yetu ipate uhuru Desemba 9, 1960 imeshapita miaka 56. Katika kipindi hicho kirefu, Tanzania imepita katika hatua mbalimbali ambazo zimewezesha kuandikwa kwa historia ndefu iliyotukuka.
Baadhi ya hatua ilizopita nchi yetu zimewekwa vizuri katika kumbukumbu mbalimbali za maandishi na katika maktaba na Makumbusho ya Taifa, ambako vizazi vijavyo vitapata nafasi ya kujifunza nchi yao ilikopitia kufikia hapa iliko au itakapokuwa kwa miaka mingi ijayo.
Katika hatua zote ambazo nchi yetu imepita, wapo watu wenye umaarufu na wasiokuwa nao, ambao wako nyuma ya historia. Watu hawa ama walikuwa waasisi wa historia hiyo au waliwezesha tu iandikwe.
Mathalani, kuna mtu aliyebuni jina la Tanzania baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana Aprili 26, 1964 ambaye hafahamiki kokote na tuendako hata watu wachache wanaomjua, kama wapo, watatoweka na historia yake itafutika.
Mfano mwingine, ni mtu aliyebuni na kutunga Wimbo wa Taifa, au aliyependekeza rangi za Bendera ya Taifa na jinsi ya kuzipanga, aliyebuni na kutengeneza Mwenge wa Uhuru na wengine wengi ambao historia halisi ya nchi haiwezi kuandikwa pasipo kukumbuka ubunifu wao.
Umuhimu wa kuwakumbuka watu hao umechagizwa na suala linalovuma sasa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu Mzee Francis Maige anayedaiwa kuchora nembo ya Taifa yenye alama ya ngao ya bibi na bwana. Mtu huyo alikutwa akiwa anaumwa bila msaada.
Tunashukuru, Serikali imeamua kumpa matibabu na kumtunza mzee huyo, maarufu kwa jina la Ngosha, anayedaiwa kuchora nembo hiyo mwaka 1957. Awali, alilazwa Hospitali ya Amana na baadaye akahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla alikaririwa na gazeti hili akisema Serikali itasimamia matibabu yake na itamtunza kwa kumpa makazi yatakayomfaa.
Dk Kigwangalla alifika hospitalini hapo kutimiza azma ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambaye aliahidi bungeni kuwa Serikali itamfuatilia kwa kuwa ametoa mchango mkubwa kwa Taifa.
Kauli ya Dk Kigwangalla kuwa Serikali haikuwa na habari za mtu huyo inachochea utambi katika hoja yetu ya kuitaka iwatafute na kuwambua watu wote walioandika historia ya nchi yetu, kwa kuwa nao ni sehemu ya kumbukumbu hiyo.
Kama alivyosema Dk Kigwangalla, nembo iliyochorwa na Ngosha itaishi kwa muda mrefu na hivyo mchango wake utabaki hapa duniani hata atakapoondoka, kama ambavyo michango ya wengine wa aina yake itadumu.
Tunaungana na Dk Kigwangalla kwamba ni muda muafaka kwa Serikali kuwatafuta watu mashuhuri kama Ngosha waliofanya kazi kubwa kwa kutumia akili zao kwa ajili ya Taifa hili.
Umuhimu wa kuwaenzi watu hao ambao ni sehemu ya historia ya nchi, unaongezwa na madai yaliyoibuka sasa kuwa hata nembo hiyo haikuchorwa na Mzee Ngosha, bali ilibuniwa na Jeremiah Kabati wa Bwiru, Mwanza. Na pengine hawataishia hapo, anaweza kutokea mwingine na mwingine.
Ni kutokana na utata huo, sisi tunaamini ni wakati muafaka kwa Serikali kuainisha wanahistoria hawa na wasifu wao ili kuweka kumbukumbu sawa kuhusu mchango wao kwa Taifa.
Kuenzi watu hao kutachochea kizazi cha sasa kuona umuhimu wa kutumia ubunifu wao kwa ajili ya Taifa hili kwa kuwa mchango wao utatambulika na kuenziwa.
0 Comments