TUME ya Vyuo Vikuu imekiri kuitisha mitihani ya utambuzi wa sifa mbadala (RPL) kwa watu ambao wana uzoefu wa siku nyingi katika fani zao wanazofanyia kazi, lakini hawana vigezo vya kielimu vya kujiunga na elimu ya chuo kikuu.
TCU imesema mitihani hiyo malengo yake ni kuwawezesha watu ambao wamefanya kazi kwa siku nyingi ambao watafaulu, waweze kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika fani wanazofanyia kazi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa TCU, Edward Mkaku, alisema jana kwamba mtihani huo ni wa utambuzi wa sifa mbadala ambao unawalenga watu ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu, lakini hawana vigezo ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu.
“Kuna watu huko maofisini wana uwezo mkubwa wa kazi, wanawafundisha kazi hata watu ambao wamehitimu shahada, sasa huyo ndio tunayemlenga,” alisema Mkaku. Alisisitiza lengo la kuanzisha mitihani ya namna hiyo ni kuhakikisha kwamba watu ambao wamekaa muda mrefu kazini nao wanapata nafasi ya kujiendeleza kielimu.
“Kwa mfano kwenye vyumba vya habari huko kuna waandishi wazuri, ambao wana uwezo mkubwa wa kazi, hawa unaweza kukuta wameishia darasa la saba au kidato cha nne, lakini wamefanya kazi kwa muda mrefu, mitihani hii ni kwa ajili yao,” alisema.
Alisema cha msingi awe anajua kusoma na kuandika kiingereza, kwani ndio lugha ambayo inatumika katika kufanya mtihani huo wa RPL. Alitaja vituo vya mitihani hiyo kuwa ni Chuo Kikuu Huria, Chuo Kikuu cha Tumaini, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Tumaini cha Makumira na Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Mkaku alisema kwa wote ambao watafaulu mtihani huo, watatunukiwa cheti ambacho watakitumia kuombea kozi wanazotaka kusomea kwenye vyuo mbalimbali vya elimu ya juu. Alisema wahitaji wanaomba kwenye TCU sio kuomba kwenye chuo.
Akizungumzia tangazo linalosambaa mitandaoni, Mkaku alikana kuhusika kwa tangazo hilo kwa maelezo kuwa wale ambao wameweka namba zao za simu hawatambuliwi na tume hiyo.
“Hizo namba walizoweka hata mimi nimewatafuta, nilitaka wanisaidie wao wanahusikaje, tunaomba wahusika waingie kwenye tovuti yetu inajieleza kwa ufasaha zaidi,” alisema Mkaku.
Alipoulizwa kama mpango huo umepata kibali cha waziri wa elimu, Profesa Joyce Ndalichako, Mkaku alisema TCU ndio wanaosimamia mafunzo ya vyuo vya elimu ya juu na mpango huo una mibaraka yote ya Serikali.
“Tunatoa mwito kwa watu kuomba ili wakafanye mtihani huo, tunaamini kwamba utawasaidia watakaofaulu kupata elimu ya chuo kikuu na kuwawezesha kustaafu wakiwa na mishahara mizuri kuliko ilivyo sasa hivi wanazibiwa kwa kuwa hawana elimu ya chuo kikuu,” alifafanua.
0 Comments