SHIRIKA LA KUTETEA UHAI(PROLIFE) LAUNGA MKONO WASICHANA WANAOPATA MIMBA KUTOREJEA SHULE BAAFA YA KUJIFUNGUA.

Wanafunzi wa Sekondari ya Wasichana. Rais Magufuli amesema hataruhusu katika utawala wake wanafunzi watakaobeba ujauzito kuendelea na masomo.

SHIRIKA la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, kambi ya upinzani na wadau wengine wameunga mkono msimamo wa Rais John Magufuli kuhusu wasichana wanaopata mimba na kujifungua kutorejea shuleni kuendelea na masomo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wadau hao wamesema wanakubaliana na Rais Magufuli kwa masimamo wake kama mzazi makini na mwenye uchungu na watoto.

Mkurugenzi wa Prolife-Tanzania, Emil Hagamu alisema anaunga mkono kauli na msimamo wa Rais kwa kuwa ni mzuri na pamoja na mambo mengine, unawasaidia wazazi, walezi na viongozi wa dini kuimarisha malezi na maadili kwa watoto.

“Namuunga mkono Rais wetu; hili lilikuwa miongoni mwa malalamiko makubwa ya watu kupinga mimba za utotoni kwa sababu watoto hao bado wadogo, hivyo, hawapaswi kukubali kushiriki vitendo wanavyojua vinakiuka maadili ya jamii katika familia, shule na hata dini zao,” alisema Hagamu.

Akasisitiza, “Kuruhusu watoto wakipata ujauzito waende wajifungue kisha warudi shuleni, utakuwa umeruhusu vitendo vya ngono kwa sababu ni watoto.

“Unajua mtoto wa shule anapopata mimba, huwa na msongo na matazamio ya kuwa mama na kwamba tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu watoto waliopata mimba shuleni zinaonesha hawana matokeo mazuri shuleni,” alisema.

Kwa mujibu wa Hagamu, kauli ya Rais ikizingatiwa sambamba na maadili yanayofundishwa katika jamii na dini mbalimbali, ni wazi hata vifo na madhara yanayotokana na utoaji mimba vitapungua.

Alisema lazima maadili ya nchi na jamii yazingatiwe sambamba na kuwachukulia hatua kali zaidi wanaosababisha ujauzito kwa watoto wa shule na wenye umri wa chini ya miaka 18.

“Lazima turejeshe maadili yetu ya zamani ili watoto wetu wawe na nafasi ya kuzingatia masomo na wafanye vizuri zaidi katika masomo yao ili baadaye watumikie vema taifa, dini na familia zao,” alisema.

Mkurugenzi huyo wa Prolife alikwenda mbali na kusema, “Namshauri Rais atazame hata mfumo wa sasa wa elimu ambapo wanafunzi kuanzia darasa la tano wanafundishwa elimu inayohusisha mambo ya ngono kwa kuwa elimu hiyo kwa watoto, inahamasisha watoto kujaribu na kuangamia katika magonjwa na mimba.” “Wanasaikolojia wanasema mtoto anapofundishwa elimu inayohusu ngono mapema, ndivyo anavyoshawishika kujaribu mapema,” alisema Hagamu.

Kwa upande wa wazazi, Emerenciana Mkony mkazi wa Dar es Salaam alisema msimamo wa Rais umetazama mbali katika kujenga taifa la watu adilifu na wanaozingatia wakati wa kufanya kila jambo.

“Msimamo huu wa Magufuli ni msimamo nzuri kwa sababu ikiwa watoto wataruhusiwa kurudi shule baada ya kujifungua, maadili yatazidi kuporomoka na mwisho wa siku taifa litakosa watu wenye nidhamu,” alisema.

Kwa upande wake, Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo amesema kambi hiyo haiungi mkono suala la watoto kupata mimba wakiwa shuleni.

Aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku moja baada ya Rais John Magufuli kupiga marufuku mpango unaopigiwa debe wa kuruhusu wanafunzi wanaobeba ujauzito wakiwa shuleni waruhusiwe kurejea shuleni baada ya kujifungua.

“Sisi kama kambi ya upinzani ni kweli tunapinga kabisa na suala la watoto kupata mimba kwa maana ya kufanya mapenzi, tukiweza kuboresha elimu yetu na miundombinu ya shule zetu ni wazi tatizo hili kubwa la mimba litaweza kuepukika na hata haya tunayojadili hayatakuwepo,” alisema Lyimo.

Naye mmoja wa wadau wa elimu na maadili, Gladness Munuo alisema anaiunga mkono kauli ya Rais Magufuli kwa asilimia 100 kwani ni hatua nzuri itakayosaidia jamii kuwa na nidhamu.

“Namuunga mkono Rais, sio kwamba sitaki watoto wa kike wasome la hasha, bali hali ilikuwa mbaya; asilimia kubwa ya watoto wa kike chini ya miaka 18 walikuwa wanaacha masomo kwa sababu ya mimba, sasa ukisema unaruhusu wajifungue kisha warudi shule hapo hapatakuwa na maadili tena, bali tutazidi kuwafanya waone vitendo vya uasherati ni jambo la kawaida hata wakiwamo masomoni jambo ambalo si kweli na ni hatari kwa ustawi wa jamii,” alisema Munuo.

Munuo alisema jamii ikiungana kuziba mianya yote ya watoto kujihusisha na uasherati hata wawapo shuleni, itafanikiwa kupunguza mimba za utotoni, utoaji mimba na pia, kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kudhibiti ongezeko la watoto wa mitaani kutokana na wengine kuzaliwa na mama ambao ni watoto wenzao.

Alisema nchi imekuwa ikipiga kelele kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano na madhara ya watoto kujifungua wakiwa katika umri wa utoto.

Kwa mujibu wa Munuo, takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa miongoni mwa wanaopoteza maisha katika kujifungua, ni pamoja na wanawake wenye umri chini ya miaka 18 kwa kuwa maumbile yao hayajajiandaa kwa jukumu la uzazi.

Alisema hali hiyo inawaweka katika hatari ya kifo wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua. Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Tanzania Bara, Getrude Ndibalema, yeye alisisitiza maadili tangu katika familia na elimu zaidi kutolewa ili umma uelewe vizuri Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya Mwaka 1998 zinazozuia vitendo vya ngono na mwanafunzi au mtu mwenye umri chini ya miaka 18.

Alisisitiza kuboresha miundombinu ya elimu, maadili na usalama kwa watoto wa kike tangu nyumbani, njiani na shuleni. Habari hii imeandaliwa na Anastazia Anyimike (Dodoma), Ikunda Eric na Joseph Sabinus (Dar).

0 Comments