Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya leo amekabidhi Bendera ya Taifa kwa wanafunzi saba wanaosoma masomo ya sayansi wanaokwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya First Global Challenges nchini Marekani. Makabidhiano hayo yamefanyika katika shule ya Sekondari ya wasichana Jangwani.
Katika makabidhiano hayo Mhandisi Manyanya amewataka wanafunzi wote nchini kusoma kwa bidii masomo ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuhakikisha ndoto ya Tanzania ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda na biashara inafanikiwa na kwamba wizara tutaendelea na jukumu lake la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili wanafunzi wote waendelee kufanya vizuri katika masomo ya sayansi.
Shule zilizotoa wanafunzi watakaoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Jangwani, Azania, Jamhuri, Benjamini Mkapa, Feza na Kisutu.
Naye mratibu wa mashindano hayo kwa upande wa Tanzania ndugu Mkufu Shabani Tindi alisema mashindano haya yameanzishwa na kufadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Marekani liitwalo FIRST yenye maana ya for inspiration and recognition of science and technology lenye lengo la kuhamasisha ulimwenguni kote vijana wanaosoma masomo ya sayansi, uhandisi, teknolojia na hesabu kuweza kutatua changamoto mbalimbali ulimwenguni
Wanafunzi watakaoshiriki wanatarajia kuondoka kesho Juni 12, 2017 na watakuwa nchini Marekani kwa ajilia ya mashindano hayo makubwa kiulimwengu ambapo zaidi ya nchi 170 zitashiriki.
Naye mmoja wa washiriki Raymond Benedict kutoka Shule ya Sekondari Jamhuri amesema yeye wenzake wamejiandaa vizuri katika kuhakikisha wanaiwakilisha nchi katika mashindano hayo vizuri na kwa ufahari.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Mhandisi Stella Manyanya akikabidhi Bendera ya Taifa kwa wanafunzi watakaoshiriki katika mashindano ya First Global Robotic Challenges nchini Marekani.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya pamoja na baadhi ya wanafunzi watakaoshiriki katika mashindano ya First Global Robotic Challenges wakiwaonyesha wanafunzi wa shule ya wasichana Jangwani (Hawapo pichini) Roboti walioibuni.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Mhandisi Stella Manyanya akipata maelezo kutoka kwa mwanafunzi Raymond Benedict kutoka shule ya sekondari Jamhuri ya namna roboti iliyobuniwa inavyofanya kazi
0 Comments