Lipo tatizo la ajira kwa vijana wengi nchini hivyo kuongeza ushindani kutokana na uzoefu na mahitaji ya taasisi zinazoajiri. Vijana wengi wanalalamika juu ya ukosefu wa ajira na kusahau kuangalia fursa nyingine zinazoweza kuwasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Mfumo wa umiliki wa biashara unaruhusu watu kuungana na kuanzisha biashara na kuimiliki kwa pamoja. Inaweza kuwa kampuni, ushirika au taasisi zisizo za serikali.
Lipo tatizo la ajira kwa vijana wengi nchini hivyo kuongeza ushindani kutokana na uzoefu na mahitaji ya taasisi zinazoajiri. Vijana wengi wanalalamika juu ya ukosefu wa ajira na kusahau kuangalia fursa nyingine zinazoweza kuwasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Kuanzisha vikundi ni moja kati ya vitu ambavyo vinaweza kuwasaidia vijana kusogea na kukua kwenye biashara au ubunifu. Wakati wa kuanzisha vikundi lazima wazingatie sifa ikiwamo kuwa na watu wenye maono na dhamira sawa, kujitolea, kukubali kufanya ya ziada kwa ajili ya kusimamia kikundi, kukubali changamoto na kubadilika kila wakati.
Umuhimu wa kufanya kazi kwenye vikundi ni mkubwa ingawa mtaji hasa wa fedha mara nyingi ni changamoto ambayo inaweza kutatuliwa kwa muunganiko wa vijana. Mkiwa wengi ni rahisi kupata mtaji mdogo wa kuanzia kwa kuunganisha nguvu na rasilimali nyingine mlizonazo.
Hii inaweza kuendelea kukua na kufanya biashara au shughuli yoyote iliyoanzishwa kufika mbali sana. Mfumo na kiasi cha uchangiaji ni makubaliano ya wana kikundi wenyewe.
Kupitia vikundi mradi wa vijana unapata rasilimali watu kwa urahisi. Biashara ndogo inayoanza inakosa uwezo wa kuajiri na kuwalipa wafanyakazi au wataalamu wa kusaidia kuendesha biashara hivyo wanakikundi wanaendelea kubeba majukumu ya uendeshaji wa shughuli zote kwa sababu kati yao wapo wenye stadi na elimu tofauti hivyo wakitumika vizuri watakuwa wananufaisha shughuli yao.
Kitu kingine kuhusu kufanya kazi kwa vikundi ni kutumia rasilimali nyingine za nje kwa pamoja. Katika kikundi mkikutana watu zaidi ya watano na kutengeneza mtandao mwingine wa watu ambao kila mmoja wenu anawafahamu unaweza kuwa mkubwa na kukuza masoko, elimu ya vitendo kutoka kwa wenye uzoefu, kufungua fursa za kusonga mbele.
Faida nyingine ya kuwa kwenye kikundi ni kupunguza woga wa majanga au kushindwa kwenye biashara. Katika kundi wapo wengine ambao hawaogopi changamoto za biashara.
Namaanisha, kuna mtu anaweza kuwa na woga kwenye uwekezaji fulani lakini kutokana na uzoefu wa wadau wengine kwenye wazo au biashara husika basi wana mtoa wasiwasi. Kama mtu angekuwa peke yake huenda ingekuwa vigumu kuuondoa wasiwasi aliokuwa nao.
Mkiwa kwenye vikundi ni rahisi kuonekana na kupata wadau watakaowasaidia kwenye mambo ya msingi kama elimu ya ujasiriamali, fedha, uwekezaji na kunufaika na mtaji wenye masharti nafuu kutoka taasisi za fedha.
Mfumo unabadilika hata huduma nyingi za watu wa kipato cha chini zinaendeshwa kwa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja. Ipo mifano ya dhahiri kwenye vikundi vya kuweka na kukopa maarufu kama Vicoba, vikundi vya uzalishaji na masoko.
Hii yote ni kwa ajili ya kukusanya nguvu za watu wengi wenye uwezo wa chini na kutengeneza msimamo na dira ya pamoja ambayo kwa kiasi kikubwa imefanikiwa na kuleta majibu chanya.
Kuwezesha vijana ndiyo wimbo unaosikika zaidi wakati huu hivyo sioni sababu ya vijana kuendelea kukaa bila kutafuta mbinu za kujikwamua ili kusogea taratibu. Nafasi na fursa ni sawa kwa wote, tutengeneze vikundi visivyobagua wanachama. Tuweke usawa na tuaminiane, tukifanya haya tunaweza kusogea na kupata majibu chanya.
0 Comments